March 7, 2026

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Rais Dkt. Mwinyi atoa pole kufuatia kifo cha Spika Mstaafu Job Ndugai

Na Mwandishi Wetu, TimesMajira Online

RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dkt. Hussein Ali Mwinyi, ameeleza masikitiko makubwa kufuatia kifo cha Spika Mstaafu wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na aliyekuwa Mbunge wa Jimbo la Kongwa, Mheshimiwa Job Yustino Ndugai, kilichotokea leo jijini Dodoma.

Katika salamu zake za rambirambi, Rais Mwinyi amesema kuwa taifa limepoteza kiongozi aliyetoa mchango mkubwa katika nyanja mbalimbali za uongozi, hususan katika mihimili ya dola, akiwa miongoni mwa wanasiasa waliotumikia taifa kwa muda mrefu kwa uzalendo na uadilifu.

“Marehemu Job Ndugai nitamkumbuka kwa mchango wake mkubwa katika uongozi wa Bunge na nafasi nyingine alizowahi kushika, ambapo alijitahidi kuimarisha utendaji na kuhakikisha masuala ya wananchi yanashughulikiwa kwa weledi,” amesema Dkt. Mwinyi.

Aidha, Rais Mwinyi ametoa salamu za pole kwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, Spika wa Bunge Dkt. Tulia Ackson Mwansasu, familia ya marehemu, wananchi wa Jimbo la Kongwa pamoja na ndugu, jamaa na marafiki wote walioguswa na msiba huo mzito.

Amesisitiza kuwa kipindi hiki cha majonzi kinahitaji uvumilivu na mshikamano, huku akiwataka wote walioguswa na msiba huo kuwa na subira na kumtanguliza Mwenyezi Mungu katika sala na maombi.

“Mwenyezi Mungu ailaze roho ya Marehemu Mahala Pema Peponi. Amina,” amesema Rais Dkt. Mwinyi.

Marehemu Job Ndugai atakumbukwa kama mmoja wa viongozi waandamizi waliolitumikia Bunge kwa miaka mingi, akipitia ngazi ya Naibu Spika hadi kuwa Spika kamili wa Bunge, nafasi aliyoishika kwa ufanisi mkubwa hadi alipojiuzulu mwaka 2022. Pia alikuwa mbunge wa Kongwa kwa zaidi ya miaka 20. Taarifa zaidi kuhusu maziko na shughuli za maombolezo zinaendelea kuratibiwa na serikali kwa kushirikiana na familia.