March 7, 2026

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Tume ya Kurekebisha Sheria yatakiwa kuangalia sheria ndogondogo za Halmashauri

Na Joyce Kasiki, TimesMajira Online ,Dodoma

Mkuu wa Wilaya ya Kongwa Mayeka Saimon, ameitaka Tume ya Kurekebisha Sheria Tanzania kuanza kuangalia kwa undani sheria ndogondogo zinazopitishwa na halmashauri na vijiji, akibainisha kuwa baadhi ya sheria hizo zinaweza kutoa mchango mkubwa katika maboresho ya sheria kuu (mama) za kitaifa.

Akizungumza katika maonyesho ya kitaifa ya Nane Nane yanayofanyika jijini Dodoma, Mkuu huyo wa wilaya alisema mara nyingi sheria hizi za maeneo ya chini zinaibua suluhisho la changamoto za moja kwa moja kwa wananchi, lakini hazifanyiwi tathmini kwa mapana yake.

“Inawezekana jambo linaonekana ni la kawaida, lakini kule chini kwenye jamii linakuwa ndiyo kero kubwa kwa wananchi. Sheria ndogo ya halmashauri moja inaweza kufanya vizuri lakini nyingine hazijui kama ipo. Mkiangalia sheria hizi zinaweza kusaidia sana katika marekebisho ya sheria mama,” amesema DC huyo.

Kwa upande wake, Wakili wa Serikali kutoka Tume ya Kurekebisha Sheria, Bi. Vicky Mbunde, amesema Tume hiyo ilianzishwa mwaka 1981 na kuanza rasmi kazi mwaka 1983 kwa lengo la kupitia, kuchambua na kupendekeza maboresho ya sheria nchini.

Ameeleza kuwa Tume hupokea maoni ya wananchi na wadau mbalimbali kuhusu sheria, na kisha kufanya mapitio ya kina ili kubaini mapungufu, ufanisi, au kutokidhi kwa sheria husika katika mazingira ya sasa.

“Tume imefanya mapitio ya sheria mbalimbali ikiwemo Sheria ya Uchaguzi ya mwaka huu, Sheria ya Mtoto na hii ni kutokana na kuongezeka kwa ukatili dhidi ya watoto, pamoja na Sheria ya Vinasaba (DNA) ambayo ilikuwa na mgawanyiko mkubwa kabla ya kutungwa,” amesema Bi. Mbunde.

Amefafanua kuwa katika sekta ya kilimo, Tume hufanya utafiti wa mfumo mzima wa sheria badala ya sheria moja tu, na kwamba tafiti hizo hujumuisha sheria zote zinazogusa moja kwa moja au kwa njia isiyo ya moja kwa moja sekta husika.

Hata hivyo, amebainisha kuwa kuna changamoto kadhaa zinazoikabili Tume katika utekelezaji wa majukumu yake, zikiwemo ufinyu wa bajeti, unaosababisha sheria chache kufanyiwa mapitio kwa mwaka licha ya kuwepo zaidi ya sheria 400 nchini.

Vile vile amesema changamoto nyingine ni uelewa mdogo wa wananchi, unaosababisha wengi wao kushindwa kutoa maoni wakati wa mchakato wa mapitio ya sheria,miundombinu hafifu ya ushirikishaji wa jamii, hasa maeneo ya vijijini.

“Kwa mwaka, tunafanya mapitio ya sheria kati ya 10 hadi 12 pekee, wakati tuna zaidi ya sheria 400. Taratibu zinatutaka kila baada ya miaka mitano sheria iwe imefanyiwa tathmini, lakini kwa sababu ya bajeti ufinyu wa bajeti hatuwezi kufanikisha hilo kwa wakati,” ameeleza.

Ameongeza kuwa kwa sasa Tume inaendelea kutumia mbinu mbalimbali za kuboresha ushirikiano na jamii ili kupokea maoni ya wananchi kwa wakati, hasa yale yanayowagusa moja kwa moja katika maisha yao ya kila siku.