March 7, 2026

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Tume ya Kurekebisha Sheria yatoa elimu kwa Tume ya Taifa ya Umwagiliaji

Na Joyce Kasiki,Timesmajira online,Dodoma

TUME ya Kurekebisha Sheria Tanzania imeendelea kutekeleza majukumu yake kwa kuzingatia ushirikishwaji wa wananchi na wadau mbalimbali wa sheria ili kuhakikisha sheria zinazotumika nchini zinaendana na wakati na mahitaji ya jamii.

Akizungumza katika maonesho ya kitaifa ya nanenane yanayoendelea jijini Dodoma wakati akitoa elimu kuhusu majukumu ya Tume hiyo , Wakili wa Serikali kutoka Tume hiyo, Bi. Vicky Mbunde amesema kuwa moja ya majukumu makuu ya Tume hiyo ni kupitia sheria, kufanya tafiti za kisheria, kufanya mapitio ya sheria ili kubaini iwapo bado zinafaa kwa mazingira ya sasa au zina mapungufu, na kutoa elimu ya sheria kwa umma.

“Sisi tuna’deal’ na sheria zote zinazotungwa na Bunge, kwa hiyo hatuwezi kuja na maoni yetu wenyewe. Lazima tushirikiane na wananchi tusikie wanasema nini kuhusiana na sheria zilizopo, na hapo ndipo tunapata maoni yao kuhusu sheria zetu,” amesema Bi. Mbunde.

Ameongeza kuwa Tume imekuwa ikishiriki katika maonyesho mbalimbali ikiwa ni sehemu ya juhudi za kuufikia umma na kutoa elimu kuhusu mchakato wa maboresho ya sheria, huku akibainisha kuwa ushirikiano wa wananchi ni nguzo muhimu katika kazi hiyo.

Kwa upande wake, Wakili wa Serikali kutoka Tume hiyo, Bw. Baraka Chipamba, ameeleza kuwa Tume inasimamia pia utekelezaji wa Sheria ya Umwagiliaji Na. 4 ya mwaka 2013 ambayo ilianzishwa baada ya kupitishwa kwa Sera ya Taifa ya Umwagiliaji ya mwaka 2010.

“Sheria hiyo ilizalisha Tume ya Taifa ya Umwagiliaji ambayo, pamoja na majukumu yake ya msingi, pia inahusika na masuala ya mazingira. Ndani ya sheria hiyo yapo makosa na makatazo ambayo wadau wanapaswa kuyafahamu na kuyazingatia,” amesema Bw. Chipamba.

Amefafanua kuwa makatazo hayo ni pamoja na uvamizi wa maeneo yaliyotengwa kwa ajili ya shughuli za umwagiliaji, matumizi ya kemikali katika vyanzo vya umwagiliaji vinavyoweza kuathiri mazao, uvuvi usio rasmi katika vyanzo vya umwagiliaji bila kibali maalum cha maandishi, na uchepushaji wa maji kinyume na taratibu zilizowekwa.

“Tunaamini kuwa vyama vya umwagiliaji vina nafasi kubwa ya kuhakikisha sheria hii inatekelezwa ipasavyo. Viongozi wa vyama hivyo wanapaswa kusaidia kusimamia matumizi sahihi ya vyanzo vya maji, ili visitumike kwa shughuli zisizo rasmi kama uvuvi au matumizi ya kemikali bila kibali,” ameongeza.

Tume ya Kurekebisha Sheria imeendelea kusisitiza kuwa mafanikio ya maboresho ya sheria nchini hayawezi kufikiwa bila ushirikiano wa karibu kati ya Serikali, wananchi na wadau wengine wa maendeleo.