March 7, 2026

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

UDSM yafanya utafiti wa nyuki wadogo,yaonyesha umuhimu wa wadudu hao

Na Joyce Kasiki,Timesmajira online,Dodoma

CHUO Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM), kimefanya utafiti wa kina kuhusu mtawanyiko na umuhimu wa nyuki wadogo nchini Tanzania, na kugundua mchango mkubwa wa viumbe hao katika uchavushaji wa mimea, uhifadhi wa mazingira na afya ya binadamu.

Utafiti huo, ambao umefanywa katika maeneo mbalimbali nchini, umebaini kwamba Tanzania ina jumla ya aina 12 za nyuki wadogo kati ya aina 33 zilizopo Afrika, huku dunia nzima ikiwa na takriban aina 605 za nyuki hao wanaopatikana zaidi kwenye maeneo ya kitropiki.

Hayo yamesema na Mwanasayansi Kutoka UDSM ambapo amesema “nyuki wadogo ni viumbe muhimu sana katika mfumo wa ikolojia. Wana uwezo wa kutembelea maua yenye ukubwa tofauti, hivyo kusaidia katika uchavushaji wa mimea mbalimbali,” alisema Bw. Mwambogela alipokuwa akiwasilisha matokeo ya tafiti hizo katika maonesho ya kisayansi ya UDSM.

Amesema ,uchavushaji huo husaidia mimea kuzalisha kwa wingi, na hivyo kuchangia usalama wa chakula na bayoanuwai. Mbali na uchavushaji, asali inayozalishwa na nyuki hao imeonekana kuwa na virutubisho vingi zaidi kutokana na wingi wa maua wanayotembelea, hivyo kuwa na uwezo mkubwa wa kusaidia matibabu ya magonjwa mbalimbali.

Katika maeneo ya ukanda wa mashariki, tafiti zimeonesha kuwa kuna wingi wa nyuki wadogo kuliko kanda nyingine, jambo linaloonesha kuwa mazingira ya maeneo hayo ni rafiki kwa maisha ya nyuki hao.

Hata hivyo, Bw. Mwambogela ameonya kuhusu changamoto ya kupungua kwa idadi ya wadudu wachavushaji duniani, hali inayohatarisha uzalishaji wa mazao na ustawi wa mazingira. “Ili kuwalinda, ni muhimu kujua wanapatikana wapi, na pia kuelimisha jamii kuhusu faida zao,” alisisitiza.

Katika baadhi ya maeneo, wananchi wamekuwa na imani potofu kuhusu nyuki hao, wakiamini kuwa ni “nyuki wa laana” na kutumia asali yao kwa madhumuni potofu kama kuharisha au kutoa mimba. Hata hivyo, baada ya kupewa elimu na watafiti wa UDSM, baadhi yao wameacha imani hizo potofu na kuanza kuelewa umuhimu wa nyuki hao katika maisha yao ya kila siku.

“Elimu ni silaha baada ya mafunzo, jamii zimeanza kubadilika na kuacha kuwatenga nyuki hawa. Wanatambua kuwa si laana bali msaada mkubwa kwa afya na mazingira,” aliongeza Bw. Mwambogela.

UDSM kupitia tafiti zake inatoa wito kwa serikali, wanazuoni na jamii kushirikiana katika kulinda na kuhifadhi nyuki wadogo, kwa manufaa ya sasa na vizazi vijavyo.

Tafiti hizi zimekuja wakati dunia inazidi kukumbwa na mabadiliko ya tabianchi, hali inayozidi kuhatarisha viumbe wachavushaji kama nyuki.