March 7, 2026

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Vyombo vya habari vyatakiwa kuripoti uchaguzi kwa weledi

Na Rose Itono, Timesmajira Online

TUME Huru ya Taifa ya Uchaguzi (INEC), imevitaka vyombo vya habari nchini, kuwa makini katika kuripoti taarifa zinazohusu Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2025.

Katika kuripoti huko, vyombo vya habari vimetakiwa kuhakikisha vinazingatia ukweli, wakati na maadili ya taaluma ya uandishi wa habari ili kulinda amani na mshikamano wa kitaifa.

Pia, Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi, imesajili Taasisi na Asasi 164, kwa ajili ya kutoa elimu ya mpiga kura katika kipindi cha kuelekea uchaguzi mkuu wa mwaka 2025 unaotarajiwa kufanyika mwezi Oktoba, mwaka huu.

Hayo ameyasema leo Mwenyekiti wa Tume hiyo, Jaji wa Mahakama ya Rufani Jacobs Mwambegele, wakati wa ufunguzi wa Mkutano wa Kitaifa wa Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi na Waandishi wa Habari jijini Dare es Salaam.

Jaji Jacobs Mwambegelege amesema, mbali na taasisi na asasi 164 kusajiliwa kwa ajili ya kutoa elimu ya mpiga kura katika kipindi cha kuelekea uchaguzi mkuu, pia taasisi na asasi nyingine 88 zimesajiliwa kwa ajili ya uangalizi wa uchaguzi

“Jumla ya taasisi na asasi 164 zimepewa kibali cha kutoa elimu ya mpiga kura, kati ya taasisi na asasi hizo 161 zimepewa kibali cha kutoa elimu ya mpiga kura kwa upande wa Tanzania Bara na tatu kwa upande wa Zanzibar,” amesema Jaji Mwambegelege

Aidha, amesisitiza kwa kuvitaka vyombo vya habari kutoa taarifa zilizo sahihi, zisizopotosha na kwa lugha ya kujenga ili kuimarisha mshikamano wa kitaifa na kulinda amani wakati wa uchaguzi.

Alisema, tume kwa kutambua umuhimu wa vyombo vya habari imeendelea kutoa mafunzo maalum kwa wahariri na waandishi wa habari kwa lengo la kuwaongezea uelewa kuhusu sheria, kanuni na taratibu za uchaguzi ili kuripoti kwa weledi na kuzuia upotoshaji.

Amehimiza wanahabari kuhimiza uvumilivu wa kisiasa kwa wananchi na kuepuka lugha zinazoweza kuchochea vurugu wakati wa kampeni ambazo zitaanza rasmi Agosti 28 na kumalizika Oktoba 28

Hata hivyo amewataka waandishi wa habari kushirikiana na tume huru ya uchaguzi kwa kuhamasisha wananchi, kuimarisha amani na kulinda mshikamano wa kitaifa.

Mshikamano huo unatakiwa kufanyika kipindi chote cha mchakato wa maandalizi ya kupiga kura bila kusahau kutunia kalamu zao kuhamasisha jamii kujitokeza kupiga kura kama kauli mbiu ya mwaka huu inayosema ,”Kura yako haki yako Jitokeze kupiga kura”.

Katika hatua nyingine, NEC imeshatangaza ratiba rasmi ya Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2025. Utoaji wa fomu kwa wagombea wa ubunge na udiwani utaanza Agosti 9 hadi Agosti 27.

Wagombea wa urais na makamu wao wanatarajiwa kuchukua fomu kati ya Agosti 14 hadi 24. Uteuzi wa wagombea wote utafanyika Agosti 27.

Kampeni za uchaguzi zitaanza Agosti 28 hadi Oktoba 27 kwa upande wa Tanzania
Bara, na hadi Oktoba 28 kwa upande wa Zanzibar.

Jaji Mwambegele aliwaasa wanahabari kutumia vyombo vyao kuhamasisha kampeni za kistaarabu zinazojenga hoja na siyo chuki au uchochezi.

“Katika kipindi hiki cha kampeni, mnapaswa kuhakikisha kuwa vyombo vyenu havitumiwi kuvuruga amani ya nchi. Toeni taarifa za haki, za kweli, na zenye kujenga jamii,” amesisitiza.