
Na Joyce Kasiki, Timesmajira online Dodoma
MKURUGENZI Mkuu wa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa Nchini (TAKUKURU), Chrispin Chalamila , amefungua rasmi kikao kazi cha wadau wa maadili jijini Dodoma huku akitoa rai kwa taasisi zote zinazohusika na usimamizi wa maadili kushirikiana kwa dhati katika kudhibiti mmomonyoko wa maadili unaochochea vitendo vya rushwa katika utumishi wa umma.
Akizungumza katika ufunguzi wa kikao hicho cha siku mbili leo Julai 30,2025 kinachowakutanisha taasisi za maadili kitaaluma pamoja na wadau mbalimbali wa utawala Bora ,Chalamila amesema, “Natoa rai kwa mawasilisho na majadiliano yenu ya kikao hiki kuwa dira ya kutuongoza katika kuboresha mifumo ya maadili ya utendaji na kitaaluma. Hii ni njia muhimu ya kuimarisha huduma katika utumishi wa umma na kukomesha vitendo vya rushwa kwa lengo la kuleta ustawi kwa wananchi.”
Kikao hicho kimebeba kaulimbiu: “Mmomonyoko wa Maadili ni Chanzo Kimojawapo cha Rushwa – Tushirikiane Kuimarisha Maadili.” Kaulimbiu hiyo imechaguliwa kutokana na ukweli kwamba ukosefu wa maadili, hasa katika ngazi ya familia na jamii kwa ujumla, ndiyo chimbuko la matatizo mengi ya kijamii, yakiwemo rushwa kazini na kwenye maeneo mengine ya huduma kwa umma.
Katika hotuba yake, Mkurugenzi Mkuu huyo amezikumbusha taasisi husika kuhusu wajibu wao wa kisheria wa kusimamia maadili ya watumishi wa umma kama ilivyoainishwa katika Kifungu cha 8(3) cha Sheria ya Utumishi wa Umma, Sura ya 298, akisema kuwa suala hilo ni mtambuka na linahitaji ushirikiano wa dhati baina ya taasisi zote za serikali na zile za taaluma.
“Naomba kikao hiki kione tatizo la mmomonyoko wa maadili kwa mapana yake na kuibua mikakati ya pamoja ya kuimarisha nidhamu kazini. Ni muhimu tuchukue hatua kwa wale wachache wanaokiuka taratibu zilizowekwa,” alisisitiza.
Aidha, ametoa wito kwa taasisi za maadili kuendelea kushirikiana na kuwekeza katika mikakati itakayoboresha utendaji wa wataalam wanaotoa huduma kwa wananchi, ikiwa ni sehemu ya kufanikisha dhamira ya Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan ya kuwa na utumishi wa umma wenye usikivu, uwajibikaji wa hiari, na uliolenga maendeleo ya Taifa.
Katika siku mbili za kikao kazi hicho, washiriki wanatarajiwa kupokea taarifa za utekelezaji kutoka kwa taasisi mbalimbali zinazohusika na usimamizi wa maadili ya kitaaluma pamoja na kufanya mawasilisho na mijadala kuhusu changamoto na mafanikio yaliyopatikana katika kudumisha maadili ndani ya taasisi zao.
Kwa mujibu wa waandaaji, lengo kuu la kikao hicho ni kujenga uelewa wa pamoja juu ya nafasi ya maadili katika kuzuia rushwa na kukuza utawala bora, huku likihimiza uundwaji wa mikakati madhubuti itakayowezesha utekelezaji wa sera na sheria za maadili kwa ufanisi zaidi.

More Stories
Usajili wa Laini za Simu: Jilinde Dhidi ya Kutumiwa Vibaya kwa Utambulisho Wako
TTCL yaadhimisha siku ya Wanawake kwa kutoa msaada JKCI
Wananchi Dodoma washauri TBA kujenga nyumba za kupangisha watu binafsi