Na Joyce Kasiki,Timesmajira online
OFISI ya Taifa ya Takwimu (NBS) imetumia jukwaa la maonyesho ya 49 ya Kimataifa ya Biashara 2025 kama fursa ya kutoa elimu na kuhamasisha matumizi ya takwimu rasmi kwa maendeleo ya Taifa huku ikieleza namna ambavyo takwimu zinazozalishwa nchini zinavyoweza kuwa chachu ya mipango bora ya maendeleo.
Akizungumza na waandishi wa habari Julai 13,2025 kwenye maonyesho hayo jijini Dar Es Salaam ,Mtaalamu wa Mfumo wa Taifa wa Kijiografia kutoka NBS Andrew Gondwe amesema kuwa kitengo hicho huzalisha takwimu mbalimbali zenye sura ya kijiografia ikiwa ni pamoja na huduma za kijamii kama elimu, afya, maji, benki, pamoja na miundombinu mingine. Takwimu hizi, amesema, ni msingi wa kupanga mipango ya maendeleo katika sekta zote.
“Tunazalisha takwimu za kijiografia ambazo ni muhimu kwa taasisi za serikali, sekta binafsi, na wadau wengine wa maendeleo na wananchi kwa ujumla,tunawahamasisha wadau wote kufika katika ofisi zetu ili wajionee jinsi takwimu hizi zinavyoweza kutumika kuboresha maisha yao na kupanga maendeleo,” amesema Gondwe.
Amesema,takwimu hizo zinazozalishwa kwa lengo la kuchochea mabadiliko lakini pia zinaonesha, kwa mfano, hali ya upatikanaji wa huduma za kijamii kama shule na hospitali, au upatikanaji wa huduma za kifedha, hali ya matumizi ya nishati safi na hivyo kuiwezesha Serikali kupanga mipango na kutekeleza kufuatia takwimu husika.
Aidha Gondwe amesema,kwa sasa, tafiti mbalimbali zinaendelea kufanyika nchini, zikiwemo za Watu wenye uwezo wa kufanya Kazi ambao unakusanya taarifa kuhusu nguvu kazi nchini, ikiwa ni pamoja na umri, jinsia, na maeneo wanayoishi ambapo amesema matokeo yake yatasaidia serikali kupanga programu za kuongeza ajira na kukuza uchumi.
Amesema utafiti mwingine ni wa Mapato na Matumizi ya Kaya Binafsi ambao ni muhimu na unalenga kupima hali ya ustawi wa jamii, upatikanaji wa huduma za kijamii, na kiwango cha umasikini. Matokeo yake yatasaidia kupanga bajeti na sera sahihi za kiuchumi. Utafiti wa mwisho ulifanyika 2018, na huu wa sasa unalenga kutoa picha ya sasa zaidi.
“Vile vile utafiti wa takwimu za Mfumuko wa Bei na Uchumi wa Taifa ambazo hutumika kupima hali ya uchumi na kusaidia kupanga bajeti, kukokotoa pato la taifa, na kuelewa mwenendo wa mfumuko wa bei unaogusa maisha ya kila siku ya wananchi.
Kwa upande wake Afisa Masoko Mwandamizi wa NBS Andrew Punjila ameongeza kuwa takwimu kutoka sensa ya watu na makazi zinatoa picha halisi ya watu nchini kwa umri, jinsi, zinaangazia watu wenye ulemavu, hali ya makazi na aina ya nishati wanayotumia.
“Kwa mfano, taarifa hizi zinaonesha maeneo yenye uhaba wa huduma za elimu kwa watoto wa shule, au maeneo yanayokumbwa zaidi na ukataji miti,” amesema Punjila.
Ameeleza kuwa kutokana na ongezeko la matumizi ya kuni na mkaa, serikali imeanzisha mikakati ya kuhamasisha matumizi ya nishati safi.
“Takwimu kuhusu uoto wa asili zinaonesha hali ilivyokuwa kati ya mwaka 2002 hadi 2022, na zinadhihirisha mabadiliko makubwa yanayosababishwa na shughuli za binadamu. Tunasisitiza kuwa matumizi ya takwimu haya yanasaidia kujua wapi pa kuwekeza nguvu zaidi katika kuhifadhi mazingira na kuimarisha huduma za kijamii,” ameongeza.
NBS imeendelea kutoa wito kwa wanahabari, watafiti, wawekezaji, na wananchi kwa ujumla kutumia takwimu rasmi katika kuandika taarifa, kupanga miradi ya maendeleo, na kufanya maamuzi ya uwekezaji.
“Hata waandishi wa habari mnaweza kutumia takwimu hizi kutengeneza habari zenye msingi imara, za kitaalamu, na zenye kuelimisha jamii,” amesema Punjila.

More Stories
Usajili wa Laini za Simu: Jilinde Dhidi ya Kutumiwa Vibaya kwa Utambulisho Wako
TTCL yaadhimisha siku ya Wanawake kwa kutoa msaada JKCI
Wananchi Dodoma washauri TBA kujenga nyumba za kupangisha watu binafsi