*Kongamano kufanyika SAUT Mwanza
*Kuwakutanisha washiriki zaidi ya 300
Judith Ferdinand, Timesmajira Online -Mwanza
Kongamano la kujadili nafasi ya ubia katika kufikia malengo ya Dira ya Taifa ya Maendeleo ya 2050,linatarajia kufanyika Julai 26,2025, katika Chuo cha Mtakatifu Agustino (SAUT), mkoani Mwanza,likiwa ni muendelezo wa kongamano la kwanza lililofanyika Chuo Kikuu cha Dar-es-Salaam Mei, 2025 kabla ya kuzinduliwa kwa dira hiyo.
Ambapo zaidi ya watu 300,wanatarajia kushiriki katika kongamano hilo,ambalo limeratibiwa kwa ushirikiano kati ya Mpango wa Utafiti na Elimu ya Demokrasia Tanzania (REDET) na Kituo cha Ubia kati ya Sekta ya Umma na Binafsi (PPPC).

Akizungumza na waandishi wa habari Julai 25, 2025 ,katika chuo SAUT jijini Mwanza, Mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Dar-es-Salaam,Idara ya Sayansi na Siasa,Dkt. Lupa Ramadhani, amesema,katika kongamano hilo kutakuwa na mada mbalimbali ikiwemo ya dhana ya PPP na nafasi yake kufikia dira ya taifa 2050.
Mada nyingine ni nafasi ya PPP katika kukuza uwekezaji na ufanisi katika uendeshaji wa Serikali za Mitaa pamoja na nafasi ya sekta binafsi na mitaji kutoka nje katika ujenzi wa uchumi wa Tanzania,ambapo wachokoza mada watakuwa ni Mkurugenzi Mtendaji wa PPPC, David Kafulila, Dkt. Jasinta Msamula na Dkt. Delphine Kessy.
Pia watakaojadili mada ni Profesa Tibaijuka, Dkt. Ponsian Ntui, Erastus Malai ambao washiriki kutoka serikalini na sekta binafsi pamoja na wananchi watashiriki kwa kutoa michango yao.
‘Kongamano hili ni utekelezaji wa malengo ya dira inayotaka watu wawezeshwe kuingia na kushiriki katika maendeleo ya taifa.Tunataka tujadiliane kwa uwazi,wiki iliyopita,dira ya maendeleo ya 2050,ilizinduliwa na Rais Samia Suluhu Hassan,na msisitizo umewekwa katika nafasi ya ubia,na dira ile inataka kila Mtanzania kushiriki katika kuleta maendeleo ya nchi yake,”amesema Dkt.Ramadhani.

Mkuu wa Kitengo cha Habari wa PPPC, Chelu Matuzya, amesema maandalizi ya kongamano hilo yamekamilika na linatarajiwa kutoa mchango katika kuongeza uelewa kuhusu nafasi ya ubia kwa maendeleo ya taifa.

More Stories
Wanawake LGTI waadhimisha siku ya wanawake Ngorongoro
Bilioni 7 kuwainua vijana 308 sekta ya uvuvi
Clara:Miaka 50 ya Sabasaba fursa mpya za Biashara na Uwekezaji