March 7, 2026

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Anzia Ulipo sasa yajikita Kanda ya Kaskazini

Na Mwandishi Wetu, Timesmajira Online

KAMPUNI ya mawasiliano ya Yas imezindua rasmi kampeni yake ya ‘Anzia Ulipo’ jijini Arusha, ikilenga kuwahamasisha wakazi wa Kanda ya Kaskazini, kwa ajili ya kugusa maisha ya Watanzania na kuchochea ukuaji wa biashara ndogo na kunwa.

Lakini pia, kuthibitisha dhamira ya Yas na Mixx, kuhakikisha kuwa kila Mtanzania anapata nafasi ya kufanikiwa kupitia teknolojia.

Akizungumza katika hafla fupi mara baada ya kuzindua ‘Anzia Ulipo’ jijini Arusha, Mkurugenzi wa Yas Kanda ya Kaskazini, Henry Kinabo amesema maendeleo ya kweli ni yale yanayomgusa kila mtu bila kumwacha yeyote nyuma.

“Yas imekuwa mstari wa mbele katika kutambulisha kampeni na promosheni zinazogusa maisha ya watanzania moja kwamoja tukichochea ukuaji wa biashara ndogo na kubwa.

“Tunaamini kwa dhati kwamba maendeleo ya kweli ni yale yanayomgusa kila mtu bila kumwacha yeyote nyuma.

“Hivyo, tunapozindua kampeni ya Anzia Ulipo hapa jijini Arusha na kwa wakazi wote wa Kanda ya Kaskazini, tunathibitisha dhamira ya Yas na Mixx ya kuhakikisha kuwa kila Mtanzania anapata nafasi ya kufanikiwa kupitia teknolojia,” amesema Henry Kinabo.

Amesema, kupitia kampeni hiyo, wanatoa wito mahsusi kwa kila Mtanzania kuziona fursa zilizopo katika ulimwengu wa kidijitali na kuzichangamkia.

Aidha, amesema Yas inawahamasisha Watanzania kuanza safari yao ya mafanikio kwa kutumia kile walicho nacho – iwe ni kipaji, ujuzi, au hata wazo zuri bila kungoja wakati maalum.

“Tunawakumbusha Watanzania kuwa mafanikio hayahitaji ukamilifu bali uthubutu wa kuchukua hatua ya kwanza.Sisi Yas, tunaamini kwenye nguvu ya teknolojia.

“Tunakupa huduma na bidhaa mahsusi zitakazoendana na safari yako ya mafanikio. Tumewekeza katika mtandao wa kisasa wa 4G na 5G unaopatikana kila kona ya nchi, tayari kukusaidia kupiga hatua yako ya kwanza,” amesema.

Hata hivyo alisema, katika mazingira ambayo ajira rasmi bado ni changamoto, vijana wengi wamechagua ujasiriamali – si kwa sababu hawana njia nyingine, bali kwa sababu wana ndoto na malengo makubwa.

“Tumeshuhudia ongezeko la biashara zinazoendeshwa mtandaoni – kuanzia kilimo kidijitali, ubunifu wa mavazi, utengenezaji wa maudhui na huduma nyingine nyingi.

“Haya yote yakiongozwa na vijana waliothubutu kufikiri tofauti – wakitumia teknolojia kama chombo chao cha mafanikio,” amesema Kinabo.

Kampeni ya ‘Anzia Ulipo’ Kwa wakazi wa Kanda ya Kaskazini itajikita Arusha, Kilimanjaro na Manyara. ‘Sisi Yas tunasema wakati wako,wangu na wetu ni Sasa’.