Na Mwandishi wetu,Timesmajira
Katibu Mtendaji wa Baraza la Taifa la Biashara (TNBC), Dkt. Goodwill Wanga, amewaalika wawekezaji kutoka Urusi kuwekeza nchini katika sekta ya uongezaji thamani wa madini ya kimkakati ya urani (uranium), ili kusaidia nchi kupata teknolojia, kutoa ajira, na kuchochea ukuaji wa uchumi.
Ameyasema hayo katika Siku ya Taifa la Urusi iliyoadhimishwa katika Maonesho ya 49 ya Sabasaba, ambapo taifa hilo limepata fursa ya kunadi maeneo ya ushirikiano wa kibiashara na uwekezaji.
Akizungumza katika maadhimisho hayo, Dkt. Wanga alisema nchi ya Urusi imepiga hatua katika matumizi ya teknolojia, hususani katika teknolojia za uchimbaji wa gesi. Hivyo, wakiwekeza kiwanda nchini, itasaidia Tanzania kupiga hatua kwa haraka kutokana na mtandao mkubwa wa biashara wa nchi hiyo.
Amesema serikali inawataka wawezekezaji kutoka nchini Urusi kuchangamkia fursa za uwekezaji zilizopo katika maeneo ya kimkakati ikiwemo gesi asilia, uzalishaji wa simu janja na teknolokia ya kidijitali.

“Tanzania ina utajiri mkubwa wa gesi asilia ambao bado haujatumiwa ipasavyo. Tunataka kushirikiana na kampuni za Urusi zenye uzoefu ili kukuza sekta hii kwa ajili ya uzalishaji wa umeme na uchakataji wa viwandani.
“Urusi ina makampuni makubwa ya nishati yenye uzoefu na mafanikio tunayohitaji. Tuko tayari kwa ushirikiano utakaoleta mafanikio ya pamoja,”amesema
Dk Wanga pia amesisitiza umuhimu wa kuanzisha viwanda vya kuunganisha simu za mkononi nchini hasa wakati huu ambapo Tanzania imeanza safari ya mabadiliko ya kidijitali ya miaka kumi.
Amesema Serikali inatoa vivutio vya kikodi na visivyo vya kikodi kwa wawekezaji watakaowekeza katika uzalishaji wa vifaa vya kidijitali.

“Kutokana na ongezeko la mahitaji ya vifaa vya kidijitali, kuanzisha kiwanda cha kuunganisha simu ni jambo la kimkakati. Tuko tayari kuwasaidia wawekezaji katika eneo hili,” amesema.
Kwa upande wake, mwakilishi wa Urusi nchini Tanzania, Nikita Rassokhih, ametaka Siku ya Urusi ifanywe kuwa sehemu ya kudumu ya maonesho ya Sabasaba akisisitiza umuhimu wake katika kukuza mazungumzo ya kibiashara.
“Maadhimisho haya yanawakutanisha wafanyabiashara wa mataifa haya mawili. Urusi iko tayari pia kuunga mkono Dira ya Maendeleo ya Tanzania ya mwaka 2050,” amesema.
Naye Lulu Mkude kutoka TanTrade alihakikishia kuwa taasisi hiyo itaendelea kuunga mkono ushirikiano wa kimataifa na juhudi za kuvutia wawekezaji.
“Maonesho ya DITF ya mwaka huu yamevutia zaidi ya washiriki 5,000 kutoka nchi 23. Tunawahimiza wajumbe kutoka Urusi kushirikiana na wafanyabiashara wa hapa nchini na kuchunguza fursa mbalimbali zilizopo,” amesema.
Juhudi hizi za kuhamasisha uwekezaji kutoka Urusi zinaendana na ajenda ya Tanzania ya kujenga uchumi shirikishi na wenye utofauti kupitia ukuaji wa viwanda, maendeleo ya kiteknolojia, na uwekezaji wa kigeni.

More Stories
Bilioni 7 kuwainua vijana 308 sekta ya uvuvi
Clara:Miaka 50 ya Sabasaba fursa mpya za Biashara na Uwekezaji
Usajili wa Laini za Simu: Jilinde Dhidi ya Kutumiwa Vibaya kwa Utambulisho Wako