March 7, 2026

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Kiwango upatikanaji wa maji Tanga kimeongezeka hadi asilimia 79

Na Zena Mohamed,Timesmajiraonline,Dodoma

IMEELEZWA kuwa kiwango cha upatikanaji maji katika Mkoa wa Tanga kimeongezeka kutoka 54%  hadi kufikia 79% na katika maeneo ya vijijini kimeongezeka kutoka 49.7% hadi kufikia 75% na miundombinu imefikia 95% mwaka  2020 hadi kufika mwaka 2025.

Hayo yameelezwa na Mkuu wa Mkoa huo Balozi Dkt.Batilda Burian wakati akizungumza na waandishi wa habari kuhusu mafanikio ya Serikali ya Awamu ya Sita.

Amefafanua kuwa Kiwango cha upatikanaji wa huduma ya maji katika maeneo yanayohudumiwa  na Mamlaka za maji HTM kimeongezeka hadi kufikia 71.9%, Mamlaka ya Maji Mji mdogo wa Songe – Kilindi kufikia 59.6% Mamlaka ya Maji Mji mdogo wa Lushoto kufikia 68.66% na Mamlaka ya maji Tanga UWASA kufikia 95%  hadi Januari, 2024.

“Idadi ya vijiji vinavyopata huduma ya maji imeongezeka kutoka vijiji 476 mwaka 2020 hadi kufikia vijiji 601 mwaka 2025.
Jumla ya miradi 151 imetekelezwa kupitia RUWASA ambapo katika miradi hiyo miradi 96 imetekelezwa na kukamilika na inatoa huduma, miradi 65 yenye thamani ya Shilingi 88,567,399,016.47 inaendelea na utekelezaji katika maeneo ya vijijini na mabwawa ya maji mawili yamejengwa na kukamilika Handeni 1 na Mkinga 1,”amesema.

Akizungumzia mafanikio katika sekta ya Umeme Balozi Dkt.Batilda amesema kiwa jumla ya Vitongoji 2382 vimefikiwa na huduma ya umeme kati ya vitongoji 4531 vya mkoa wa Tanga ikiwa ni sawa na asilimia 52.6 ya vitongoji vyote.

“Sambamba na miradi inayotekelezwa, wakala umepanga kufikisha umeme katika vitongoji 180 kupitia mradi wa HEP 2A ambapo Mkandarasi amepatikana mwezi April, 2025 na pia vitongoji 673 viko katika mpango wa kufikishiwa umeme kupitia mradi wa vitongoji HEP 2B unaotegemewa kuanza utekelezaji wake katika kipindi cha mwaka wa fedha 2025/2026,”amesema.

Aidha amesema kwa kipindi cha mwaka 2020 hadi 2025 idadi ya wananchi wanaotumia umeme imeongezeka kutoka 145,496 mpaka kufikia 248,213 ikiwa ni ongezeko la asilimia 41.4.

Pamoja na hayo amesema kuwa
Mkoa huo umeanzisha ushirikiano na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar kuhakikisha wanaongeza uzalishaji wenye tija katika mazao ya viungo vya mdalasini, iliki, karafuu, na pilipili manga kupitia Zanzibar State Trading Corporation (ZSTC).

“Mpango huu unalenga kuimarisha ushirikiano wa masoko na viwanda vya usindikaji wa mazao ya viungo vilivyopo. Kwa sasa uzalishaji wa viungo kwa mkoa ni tani 4,016 ambazo zinaingiza kwenye mkoa kiasi cha shilingi 42,106,000,000.00 kwa mwaka,”amesema.

Kwenye sekta ya Barabara amesema kuwa Mkoa huo Mtandao wa barabara wa Wakala ya Barabara (TANROADS) uliongezeka kutoka km 1,528.54 mwaka 2007 hadi km 1,809.30 za sasa ikiwa ni ongezeko la km 280.76.