March 7, 2026

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Kikwete aipongeza Serikali kwa hatua kubwa iliyopiga sekta ya elimu

Na Penina Malundo,Timesmajira

Rais mstaafu wa Awamu ya Nne, Dkt. Jakaya Kikwete ameipongeza serikali ya awamu ya sita kwa jitihada na hatua kubwa iliyopigwa kwenye elimu kwani kumekuwa na ongezeko la wanafunzi katika ngazi za awali, msingi na sekondari, pamoja na kuongezeka kwa ufaulu. 

Pia amesema Tanzania ni miongoni mwa nchi 91 zinazoshirikiana na Shirika la Global Partnership for Education (GPE) tangu mwaka na katika kipindi hicho Dola Milioni 344 sawa na zaidi ya Bilioni 894 zimetumika nchini katika kusaidia sekta ya elimu nchini.Akizungumza 

Aliyasema hayo jana jijini Dar es Salaam wakati wa  ziara ya shirika hilo na Malala Fund katika Shule ya Sekondari Kibasila, Temeke  alisema shirika hilo la GPE ambalo lipo  katika  mataifa saba tajiri duniani kwa ajili ya kusaidia nchi zinazoendelea katika sekta ya elimu.

Amesema shirika hilo bado litaendelea kusaidia na zipo Dola Milioni 88 sawa na zaidi ya Bilioni 233 za Kitanzania zitatolewa na shirika hilo.

“Katika programu hii bado zipo Dola Milioni 88 zipo kwa ajili ya shughuli hizi za elimu Tanzania, na mwaka ujao 2026 tutaanza programu inayofuatia na zitakuja fedha nyingi kwa ajili ya sekta ya elimu nchini,” Amesema Kikwete na kuongeza

“Malala nilimwalika kwa sababu yeye ni mshirika wetu katika masuala ya elimu na hivi sasa tunaanza kampeni ya mchango tena kwaajili ya miaka mitano ijayo, Malala tunamtegemea kwakuwa ni mmoja wa watu wanaotusaidia katika sekta ya elimu, tunafanya kazi kwa Katibu sana na Malala kwenye GPE ”amesema

Kwa upande wake Naibu Waziri wa Elimu Omary Kipanda amesema Serikali itaendelea kuboresha sekta ya elimu na kuhakikisha mtoto wa kike anapata elimu bora ili kuweza kutimiza ndoto zake.

Naye Mwanzilishi wa Malala Fund na mshindi wa Tuzo ya Amani ya Nobel, Malala Yousafzai amesisitiza kuwa mtoto wa kike ana haki ya kupata elimu na kutimiza ndoto zake. 

Amesema ni muhimu Serikali, mashirika ya kimataifa na jamii kwa ujumla kushirikiana katika uhakikisha kila msichana anapata haki ya elimu na kutimiza ndoto zake.

Aidha Malala katika Shule hiyo ya Sekondari Kibasila amejionea miradi mbalimbali ya elimu inayotekelezwa na Serikali kwa kushirikiana na wadau kama GPE, kwa lengo la kumwezesha mtoto wa kike kupata elimu katika mazingira rafiki.

Miongoni mwa miradi hiyo ni ujenzi wa bweni la wasichana lenye uwezo wa wanafunzi zaidi ya 200, bwalo la chakula, mradi wa utunzaji mazingira kwa wasichana na mafunzo ya ufundi wa cherehani.