March 7, 2026

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Mashine ya “Rafiki Planter” kuongeza tija kwa wakulima vijijini

Na Joyce Kasiki, TimesMajira

Katika juhudi za kuongeza tija na kuhamasisha vijana kuingia katika sekta ya kilimo, Watafiti kutoka Taasisi ya Utafiti wa Kilimo (TARI) kituo cha Ukirigulu Mwanza , wamebuni mashine mpya ya kupandia inayojulikana kama “Rafiki Planter.”

Mashine hii rahisi na bunifu imeundwa kwa mfano wa bajaji, na ina uwezo wa kupanda mazao kama alizeti, mahindi, na pamba kwa kutumia lita moja tu ya mafuta ya petroli kwa ekari moja.

Akizungumza katika maonyesho ya 49 ya Kimataifa ya Biashara yanaoyoendelea jijini Dar es Salaam  Mtafiti kutoka  TARI Ukirigulu , Dauson Malela amesema , mashine hiyo inaweza kupanda ekari moja kwa saa moja pekee, tofauti na mfumo wa jadi wa jembe la mkono unaohitaji watu 8 hadi 12 ambao hutumia saa 6 hadi 8 kukamilisha ekari moja.

Kwa kutumia “Rafiki Planter”, mkulima huokoa muda, gharama za ujira ambazo ni kati ya shilingi 40,000 hadi 60,000 kwa ekari, na pia huongeza kasi ya kupanda hasa wakati wa mvua za mwanzo na hivyo kuongeza tija katika uzalioshaji wa mazao na kipato cha mwananchi mmoja mmoja na hivyo kuchangia katika pato la Taifa.

“Mashine hii sio tu kwamba inaongeza ufanisi, bali pia inampa mkulima fursa ya kuwahi msimu na hata kupata kipato cha ziada kwa kuwasaidia wakulima wengine kupanda baada ya kumaliza shamba lake .”amesema Malela na kuongeza

‘Mashine hii inaendeshwa na mtu mmoja tu, hivyo inafaa kutumiwa na watu wa jinsia zote na rika zote  wanaume, wanawake na wazee na tunasema vifaa kama hivi ni kiini cha mpango wa serikali wa “Building a Better Tomorrow (BBT)”, unaolenga kuwawezesha vijana kupitia zana nyepesi na rahisi za kilimo.amsesisitiza

Malela ameishukuru serikali, hususan Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan, Waziri wa Kilimo Hussein Bashe, Mkurugenzi Mkuu wa TARI Dkt. Thomas Bwana, na Mkurugenzi wa kituo cha Ukirigulu Dkt. Sabas Saidia, kwa kuweka mazingira rafiki ya ubunifu kwa vijana.

Ameomba mashine hiyo izalishwe kwa wingi ili iwafikie wakulima wengi zaidi, na hivyo kuleta mabadiliko ya kweli kwenye sekta ya kilimo nchini.

Aidha amesema,mashine hiyo tayari imefanyiwa majaribio katika mikoa ya Morogoro, Dodoma, Singida, Simiyu na Geita, ambapo wakulima walitoa maoni yao na maboresho yalifanyika ambapo TARI imeingia makubaliano na taasisi ya usambazaji wa zana vijijini (KAMATECH)     , kwa ajili ya kuzalisha mashine nyingi zaidi kwa ajili ya wakulima.

Kwa mujibu wa Malela, mashine hiyo ilionekana kuvutia wakulima wengi ambapo zaidi ya wakulima 50 walionyesha nia ya kuinunua. TARI pia inapanga kuzindua toleo kubwa zaidi la mashine hiyo lenye injini ya cc 300 litakalokuwa na uwezo wa kulima zaidi ya ekari 50 kwa siku.