Na Joyce Kasiki – TimesMajira Online
MAMLAKA ya Serikali Mtandao (eGA) imeendelea kuonyesha mafanikio makubwa katika kuboresha utoaji wa huduma kwa wananchi kupitia TEHAMA, kufuatia mfumo wake wa e-Mrejesho kutwaa tuzo ya Kimataifa katika Mkutano wa Dunia wa Jumuiya ya TEHAMA (World Summit on the Information Society – WSIS 2025) uliofanyika hivi karibuni.
Tuzo hiyo ya kiheshima ilitolewa Julai 7, 2025, ambapo Tanzania kupitia toleo la pili la mfumo wa e-Mrejesho ilitangazwa mshindi katika kipengele cha Serikali Mtandao, ikiwa ni uthibitisho wa ubora wa mfumo huo katika kuimarisha uwazi, uwajibikaji na ushirikishwaji wa wananchi katika utendaji wa Serikali.
Akizungumza na waandishi wa habari kwenye banda la eGA katika maonesho 49 ya Kimataifa yanayoendelea jijini Dar es Salam, Meneja Mawasiliano wa eGA, Subira Kaswaga, alieleza kuwa ushindi huo ni matokeo ya kazi kubwa ya ubunifu na ushirikiano kati ya eGA na taasisi mbalimbali za serikali.
“Kama mfumo wetu umepata tuzo, maana yake umetambulika duniani. Huu ni ushahidi kuwa Tanzania tunaweza kutumia TEHAMA kuboresha utawala bora na utoaji wa huduma kwa wananchi,” alisema Bi. Kaswaga.
Mfumo wa e-Mrejesho – Daraja kati ya Serikali na wananchi
Kaswaga amesema,Mfumo wa e-Mrejesho umetengenezwa ili kuwezesha wananchi kuwasilisha maoni, mapendekezo au malalamiko kuhusu huduma wanazopokea kutoka taasisi za umma pia unamwezesha mwananchi kufuatilia hatua kwa hatua majibu ya malalamiko yake, hali inayoongeza uwajibikaji kwa taasisi husika.
Wananchi wanaweza kutumia mfumo huu kwa njia mbalimbali ikiwa ni pamoja na kupiga *150*00# kisha kuchagua namba 8 na baadaye namba 2, au kupitia tovuti ya www.e-mrejesho.gov.go.tz au kwa kupakua app ya e-Mrejesho katika simu zao.
Kaswaga alisisitiza umuhimu wa mfumo huo, akieleza kuwa umeboresha kwa kiasi kikubwa ushirikiano kati ya wananchi na serikali, huku ukichochea uwazi na uwajibikaji serikalini.
Mifumo mingine inayoendeshwa na eGA
Aidha amesema,mbali na e-Mrejesho, Mamlaka ya Serikali Mtandao pia imefanikiwa kuanzisha na kuendesha mifumo mingine muhimu ya TEHAMA ambayo inarahisisha huduma za serikali kwa wananchi:
Mfumo wa Huduma za Serikali Kupitia Simu za Mkononi (M-Gov) kwa kutumia *152*00#, wananchi wanaweza kupata huduma mbalimbali za serikali, zikiwemo malipo ya umeme, maji, ada na nyinginezo hata bila kuwa na intaneti. Mfumo huu ni rafiki kwa watu wote na unatumika bure.
Mfumo wa Ubadilishanaji Taarifa Serikalini:
Mfumo huu unaziwezesha taasisi za serikali kuwasiliana na kubadilishana taarifa kwa njia ya kidigitali, hivyo kuongeza kasi ya utoaji wa huduma. Kwa mfano, sasa mwananchi akihitaji huduma kutoka NIDA, NIDA inaweza kupata taarifa za mwananchi huyo kutoka TRA moja kwa moja kupitia mfumo huo bila kuhitaji mwananchi kutembea ofisi hadi ofisi.
Mfumo wa Uthibitisho wa Utambulisho (Two-Factor Authentication) kwa lengo la kuongeza usalama wa mifumo ya serikali, eGA imeanzisha mfumo unaohitaji uthibitisho wa mara ya pili (kama OTP) kabla ya kutumia huduma au akaunti za serikali. Hii inalinda taarifa binafsi na kuhakikisha uhalali wa watumiaji.
Kituo cha utafiti na ubunifu
Ili kuendelea kujibu mabadiliko ya kasi ya teknolojia duniani Kaswaga amesema, eGA imeanzisha Kituo cha Utafiti na Ubunifu wa Serikali Mtandao ambacho kinahusisha wataalamu wa TEHAMA na wanafunzi wa vyuo vikuu kufanya tafiti, kubuni na kujaribu mifumo mipya.
“Tumeweka mazingira rafiki kwa vijana wa Kitanzania kushirikiana na wataalamu wetu kubuni suluhisho za kidigitali zinazosaidia kuboresha huduma za serikali. Teknolojia hubadilika kila siku, hatuwezi kubaki nyuma,” alisema Bi. Kaswaga.
Amesema ,kituo hicho pia kinatoa nafasi za mafunzo kwa vitendo na kujitolea kwa wanafunzi wa vyuo, ikiwa ni njia ya kukuza kizazi kipya cha wabunifu wa TEHAMA nchini.
Kaswaga ametumia nafasi hiyo kuwahamasisha wananchi waitumie mifumo hiyo si yo kwa sababu ni ya kisasa tu, bali kwa sababu inaleta mabadiliko ya kweli katika utoaji wa huduma za serikali.

More Stories
Usajili wa Laini za Simu: Jilinde Dhidi ya Kutumiwa Vibaya kwa Utambulisho Wako
TTCL yaadhimisha siku ya Wanawake kwa kutoa msaada JKCI
Wananchi Dodoma washauri TBA kujenga nyumba za kupangisha watu binafsi