Na Hamisi Miraji, Timesmajira Online
MAMLAKA ya Kudhibiti na Kupambana na Dawa za Kulevya (DCEA), imekamata shehena ya dawa mpya za kulevya zijulikanazo (New Psychoactive Substance) aina ya Mitragyna Speciosa kilogram 11,031.42.
Operesheni hiyo imefanyika Mwezi Mei hadi Julai mwaka huu, kwa kushirikiana na vyombo vingine vya dola, katika maeneo mbalimbali.

Hayo ameyasema leo, Kamishna Jenerali wa Mamlaka ya Kudhibiti na Kupambana na Dawa za Kulevya (DCEA), Aretas Lyimo alipokuwa akizungumza na Waandishi wa Habari Jijini Dar es Salaam.
Kamishna Jenera, Lyimo amesema katika kipindi hicho cha Mei hadi Julai, 2025 wamekamata dawa za kulevya jumla ya kilogramu 37,197.142.
“Tumekamata jumla ya dawa za kulevya kilogramu 37,197.142 zikiwemo dawa dawa mpya za kulevya (New Psychoactive Substance) aina ya Mitragyna Speciosa kilogram 11,031.42, bangi kilogramu 24, 873.54, mirungi kilogramu 1,274.47, skanka kilogramu 13.42, Heroin kilogramu 2.21 na Methamphetamine gramu 1.42,” amesema Kamishna Lyimo.
Aidha, amesema ukamataji huo pia, ulihusisha dawa tiba zenye asili ya kulevya aina ya Ketamine kilogramu 1.92, Fluni-trazepam (rohypnol) vidonge 1,000, lita 6 za kemikali bashirifu aina ya hydrochloric acid na uteketezaji wa ekali 1,045.5 za mashamba ya bangi.
Vilevile, Kamishna Lyimo amesema kilogram 26 za dawa za kulevya aina ya heroin, zilikuwa ziingizwe nchini kutoka nchi ya Msumbiji zilizuiwa huku watuhumiwa 64 walikamatwa wakihusishwa na dawa hizo.
Hata hivyo, Kamishna Lyimo amesema katika mkoa wa Dar es Salaam, walifanya operesheni mbalimbali ikiwemo Temeke, Zinza na Posta.

Kamishina Lyimo amesema, dawa mpya za kulevya kilogramu 11.031.42 aina ya Mitragyna Speciosa, zilikamatwa Temeke jijini Dar es Salaam, katika bandari kavu ambapo ziliingizwa nchini zikitokea nchini Sri Lanka, zilikamatwa zikiwa kwenye vifungashio vyenye chapa ndani yake kuna mbolea.
“Mitragyna Speciosa iko katika kundi la dawa mpya za kulevya zinazotokana na mimea inayofahamika kwa jina la ‘Kratom’, mmea huu unakemikali aina ya Mitrogynine na 7-Hydroxymitragynine (7-HMG), ambayo ina sifa za vichangamshi.
“Lakini pia, vinapumbaza, nyenye madhara ya kiafya kwa mtumiaji kwani uhathiri mfumo wa fahamu na kusababisha uraibu hata kupelekea vifo vya ghafla,” amesema Kamishna Lyimo.
Amesema, eneo lingine ni Posta, Dar es Salaam, walikamata watuhumiwa sita wakiwemo raia wawili wa China, waliofahamika kwa majina ya Chein Bai na Qixin Xin.

Watuhumiwa hao, walikamatwa wakisafirisha dawa za kulevya aina ya Methamphetamine gramu 1.42, dawa tiba zenye asili ya kulevya aina ya Frunitrazepam (rohypnol) vidonge 1000 na ketamine zenye uzito wa kilogram 1.92.
Mbali na juhudi hizo zote pia, Mamlaka ya Kudhibiti na Kupambana na Dawa za Kulevya (DCEA), imebaini baadhi ya waharifu wa dawa za kulevya wameanza tena kutumia maiti za binadamu kubeba dawa za kulevya maarufu kwa jina la begi.
Kamishna Lyimo, amewataka wananchi kuwa makini na kuchukua tahadhari hasa wanapotumwa au kupokea mizigo kutoka kwa watu wasiowafahamu vizuri, ni muhimu wajiridhishe na mizigo wanayosafirisha kuepuka kujikuta wakihusika katika usafirishaji wa dawa za kulevya.
Mamlaka pia, imewaomba watanzania kuendelea kuunga mkono juhudi za serikali katika kukabiliana na tatizo la dawa za kulevya, kwa kuwafichua wanaohusika.
Hata hivyo, Kamishna Lyimo amesema yoyote atakayejihusisha na uzalishaji, usambazaji wa biashara za dawa za kulevya hatua kali za kisheria zitachukuliwa dhidi yao.


More Stories
Usajili wa Laini za Simu: Jilinde Dhidi ya Kutumiwa Vibaya kwa Utambulisho Wako
TTCL yaadhimisha siku ya Wanawake kwa kutoa msaada JKCI
Wananchi Dodoma washauri TBA kujenga nyumba za kupangisha watu binafsi