Na Joyce Kasiki,Timesmajira online
JESHI la Kujenga Taifa (JKT) limeibuka mshindi wa kwanza katika kipengele cha utengenezaji wa samani bora na upambaji wa ndani kwenye Maonyesho ya 49 ya Kimataifa ya Biashara (DITF) yanayoendelea kufanyika katika Viwanja vya Sabasaba, jijini Dar es Salaam.
Mkuu wa JKT Meja Jenerali Rajabu Mabele alikabidhiwa tuzo hiyo Julai 7,2025 na Waziri wa Viwanda na Biashara Dkt.Seleman Jafo kutokana na ubunifu, ubora na uzalendo uliodhihirika katika kazi za mikono ya vijana wake, hasa kwenye kutengeneza samani imara za kisasa na upambaji wa ndani.
Akizungumza na wanahabari mara baada ya kupokea tuzo hiyo mara baada ya ufunguzi wa maonyesho hayo, Mkuu wa Jeshi la Kujenga Taifa (JKT), Meja Jenerali Rajabu Mabele, alieleza furaha yake kwa kutambuliwa kwa juhudi za vijana wa JKT wanaoshiriki kikamilifu katika ujenzi wa uchumi kupitia sekta ya viwanda vidogo na kazi za mikono.
” Samani hizi zimetengenezwa kwa kutumia rasilimali za ndani na ujuzi wa Vijana wa JKT” alisisitiza
Aliongeza kuwa mafanikio haya yanadhihirisha dhamira ya JKT katika kuunga mkono juhudi za Serikali za kukuza uchumi kupitia viwanda na ajira kwa vijana, huku akiwataka Watanzania kuunga mkono bidhaa za ndani.
Maonyesho ya mwaka huu yamebeba kaulimbiu “Tanzania Mahali Salama pa Biashara na Uwekezaji,” yakiwaleta pamoja washiriki zaidi ya 3,000 kutoka ndani na nje ya nchi, huku JKT ikionyesha ubora wake katika sekta ya utengenezaji wa samani na mapambo ya kisasa kwa mara nyingine tena.
Kwa kushinda tuzo hii, JKT imeonesha kwamba jeshi hilo halijajikita tu kwenye mafunzo ya uzalendo na ulinzi wa taifa, bali pia katika kujenga uchumi kupitia ujuzi wa vitendo na ubunifu .

More Stories
Usajili wa Laini za Simu: Jilinde Dhidi ya Kutumiwa Vibaya kwa Utambulisho Wako
TTCL yaadhimisha siku ya Wanawake kwa kutoa msaada JKCI
Wananchi Dodoma washauri TBA kujenga nyumba za kupangisha watu binafsi