March 7, 2026

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

PHPA ni kituo sahihi cha taarifa za masoko ,viuatilifu na ulinzi wa mazao

Na Joyce Kasiki,Timesmajira online

MKURUGENZI wa Mamlaka ya Afya ya Mimea na Viuatilifu (PHPA) Profesa Joseph Ndunguru, amewaasa wadau na wafanyabiashara wa masuala ya viuatilifu kufika banda la Mamlaka hiyo kwa maonyesho ya Kimataifa ya 49 ya Biashara ili waweze kupata elimu sahihi kuhusu masoko ya mazao,viuatilifu,mbegu za asili ,matumizi ya viuatilifu na teknlojia mpya za kisasa za kudhibiti visumbufu vya mazao.

Akizungumza Julai 7,2025 katika banda la Mamlaka hiyo Prof.Ndunguru amesema, “banda la PHPA kwenye maonyesho haya ya Kimataifa ya Biashara ni jukwaa muhimu kwa wakulima, wafanyabiashara, watafiti na watunga sera kupata taarifa sahihi kuhusu masoko ya mazao, matumizi ya viuatilifu, mbegu za asili na teknolojia mpya za kisasa za kudhibiti visumbufu vya mazao.” Ameongeza kuwa

“Hivyo tunakaribisha wafanyabiashara na wakulima wote waje kutembelea banda letu,hapa ndipo wanapata taarifa muhimu kuhusu masoko ya mazao yaliyofunguliwa kimataifa, taratibu za kuuza mazao nje ya nchi, aina ya vibali vinavyohitajika, na namna ya kuingiza au kusafirisha mazao kwa kufuata sheria na miongozo ya kitaifa na kimataifa.

“Na tuna taarifa muhimu kwa kila kundi. Wakulima watapata elimu ya kilimo bora, watunga sera watapata takwimu na miongozo ya kusaidia maamuzi yao, wafanyabiashara watapata taarifa za masoko, taratibu za biashara ya viuatilifu na mbegu. Hii ni nafasi ya kipekee kwa kila mdau,” alisisitiza Profesa Ndunguru.

Akizungumzia kuhusu biashara ya viuatilifu amesema, biashara ya viuatilifu nchini Tanzania haipaswi kufanywa kiholela kwani viuatilifu visipotumika kwa usahihi vinaweza kuathiri afya ya walaji na mazingira.

 “Ili mtu aweze kufanya biashara ya viuatilifu lazima apate mafunzo rasmi na kupata cheti cha kufanyia biashara hiyo. Sheria ya Afya ya Mimea na Viuatilifu inataka kila mfanyabiashara afuate miongozo na kanuni zilizowekwa ili kulinda afya ya mimea, mazingira na walaji,” alisema.

Teknolojia za kisasa za kudhibiti visumbufu vya mazao

Prof.Ndunguru amesema,miongoni mwa teknolojia zinazopatikana katika banda la PHPA ni pamoja na drone, intelligensia bandia (AI) inayotambua magonjwa ya mimea kwa haraka, na taarifa za matumizi ya ndege maalum ya Serikali iliyonunuliwa kwa zaidi ya Shilingi bilioni 6, kwa ajili ya kudhibiti ndege waharibifu wa mazao kama uwele, mtama na mpunga.

 “Ndege hii mpya ni sehemu ya jitihada za Serikali kudhibiti visumbufu vya mimea, hasa ndege aina ya kwelea kwelea ambao hushambulia mazao ya nafaka. Kwa teknolojia hizi tunalenga kuongeza tija ya kilimo na kuhakikisha kuna malighafi ya viwanda na chakula cha kutosha kwa Taifa,” alieleza.

Hifadhi ya mbegu za asili na utafiti wa nasaba

Aidha, Profesa Ndunguru alieleza kuwa PHPA kupitia Benki ya Mbegu za Asili, inahifadhi zaidi ya aina 10,000 za mbegu, zinazotumika kwa ajili ya utafiti na ubunifu wa mbegu bora zitakazohimili changamoto za mabadiliko ya tabianchi na visumbufu vya mimea.

 “Hizi mbegu za asili ni msingi wa uhakika wa chakula na tija ya kilimo. Tunazitunza kwa ajili ya matumizi ya kisayansi na uboreshaji wa kilimo cha kisasa,” alisema.

Ufanisi katika biashara za Kimataifa

Katika eneo hilo amesema,PHPA pia inafanya kazi kuhakikisha Tanzania inazingatia viwango vya kimataifa vya usalama wa mimea na mazao ili kuendelea kushiriki kwenye masoko ya kikanda na kimataifa.

Profesa Ndunguru alitoa mfano wa karibuni ambapo Jumuiya ya Ulaya (EU) iliweka sharti la kuhakikisha bakteria aina ya Zairella haipo kwenye mazao ya horticulture kutoka Tanzania.

 “Tulifanya tathmini, tukatuma ripoti rasmi kwa EU, wakairidhia na sasa tumeruhusiwa kuendelea kufanya biashara na Jumuiya ya Ulaya. Hili linaonesha kazi kubwa na nyeti inayofanywa na taasisi yetu katika kuwezesha biashara ya kimataifa,” alisema.