Na Joyce Kasiki,Timesmajira online
OFISI ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali imeeleza dhamira yake ya kuendelea kutoa ushauri wa kisheria kwa taasisi za umma katika hatua mbalimbali za uandaaji na utekelezaji wa mikataba, ili kuhakikisha mikataba hiyo inaleta tija kwa Serikali na manufaa kwa wananchi.
Aidha ofisi hiyo imekuja na huduma mpya inayolenga kutoa ushauri wa kisheria kabla matatizo hayajatokea, ili kuepuka migogoro inayoweza kuchelewesha utekelezaji wa mikataba na miradi ya maendeleo.
Naibu Mwanasheria Mkuu wa Serikali, Samwel Maneno ameyasema hayo Julai 7,2025 alipotembelea banda la Wizara ya Katiba na Sheria na kuzungumza na waandishi wa habari katika Maonesho ya 49 ya Biashara ya Kimataifa ya Sabasaba yanayoendelea katika Viwanja vya Sabasaba, Jijini Dar es Salaam.
“Tunaendelea kuzipa ushauri taasisi za umma ili kuwa na ubora wa mikataba, na kuhakikisha utekelezaji wa mikataba hiyo unafanyika kwa mujibu wa makubaliano. Hii ni hatua muhimu katika kulinda maslahi ya umma na kuimarisha uwajibikaji,” alisema Mhe. Maneno.
Akizungumzia kuhusu maonyesho hayo Maneno amesema , Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali inatumia fursa ya maonesho haya kutoa huduma kwa wananchi, ikiwa ni pamoja na ushauri wa kisheria, kushughulikia malalamiko, utatuzi wa migogoro, pamoja na kutoa elimu ya sheria hususan sheria zilizofanyiwa urekebishaji katika toleo la mwaka 2023, ambazo zimeanza kutumika rasmi kuanzia Julai Mosi 2025.
Amefafanua kuwa Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali ni chombo kilichoanzishwa kikatiba kwa lengo la kuishauri Serikali katika masuala yote ya kisheria, ikiwemo kuhakikisha kuwa mikataba inayoingiwa na Serikali inazingatia maslahi ya Taifa, sheria za ndani, na mikataba ya Kimataifa.
“Kazi kubwa tunayofanya ni kutoa ushauri wa kisheria kuhusu mikataba ya Serikali. Mikataba hii inahusisha fedha nyingi za umma, ambazo zinatokana na kodi za wananchi,kwa hiyo ni wajibu wetu kuhakikisha kuwa mikataba hiyo ni mizuri, inatekelezwa kwa mujibu wa makubaliano na inazalisha matokeo chanya kwa wananchi,” amesema Maneno.
Akieleza kuhusu maboresho yaliyofanywa, Maneno amesema Ofisi yake imebuni huduma mpya inayolenga kutoa ushauri wa kisheria kabla matatizo hayajatokea, ili kuepuka migogoro inayoweza kuchelewesha utekelezaji wa mikataba na miradi ya maendeleo.
“Tumejifunza kuwa migogoro ya kisheria huchelewesha maendeleo na kuigharimu Serikali fedha nyingi,kwa hiyo tumeweka mfumo wa kuishauri Serikali mapema kabla mikataba haijasainiwa au changamoto hazijajitokeza. Hii ni njia bora ya kulinda maslahi ya umma,” amesema.
Maneno pia amezungumzia kuhusu Juzuu ya sheria ambapo ameipongeza Serikali ya awamu ya sita kwa kufanikisha urekebishaji wa sheria kupitia kuzinduliwa kwa Juzuu za Sheria za Mwaka 2023 na kuziweka kwa urahisi kwenye tovuti ya Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali.
“Tangu mwaka 2002, sheria zetu hazijafanyiwa urekebishaji,lakini kupitia juhudi za Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan, tumefanikisha kazi hiyo kwa mara ya kwanza kwa bajeti ya Serikali. Sasa wananchi wanaweza kupata sheria hizo kwa urahisi mtandaoni,” amesema Maneno.
Katika hatua ya kuleta sheria karibu zaidi na wananchi, Maneno amesema kati ya sheria 446 zilizohakikiwa, zaidi ya sheria 300 zimeanza kupatikana kwa lugha ya Kiswahili, na mchakato wa kutafsiri nyingine unaendelea kufuatia maagizo ya Rais kwa lengo ni kuwafanya wananchi waelewe sheria kwa lugha wanayoimudu.

More Stories
Usajili wa Laini za Simu: Jilinde Dhidi ya Kutumiwa Vibaya kwa Utambulisho Wako
TTCL yaadhimisha siku ya Wanawake kwa kutoa msaada JKCI
Wananchi Dodoma washauri TBA kujenga nyumba za kupangisha watu binafsi