Na Joyce Kasiki, TimesMajira Online
WIZARA ya Kilimo imeendelea kuonesha dhamira yake ya dhati ya kuhakikisha usalama wa chakula na lishe kwa Watanzania kupitia mikakati mbalimbali ya kisasa ya kilimo na uhifadhi wa chakula, ikiwemo ujenzi wa maghala ya kisasa na matumizi ya teknolojia ya umwagiliaji.
Akizungumza na katika maonyesho ya 49 ya Kimataifa ya Biashara ya Sabasaba yanayoendelea jijini Dar es Salaam., Afisa Kilimo Mkuu kutoka Wizara ya Kilimo Margaret Natai, amesema kuwa wizara imejipanga kikamilifu kuhakikisha taifa linakuwa salama kwa chakula, kwa sasa na kwa vizazi vijavyo.
“Wizara yetu ina jukumu la msingi kuhakikisha usalama wa chakula na lishe nchini. Kwa miaka ya hivi karibuni, tumeweka mikakati madhubuti ya kuongeza uzalishaji kwa kuongeza tija katika mazao, kudhibiti upotevu wa mazao baada ya kuvuna, na kuhakikisha uhifadhi bora wa mazao,” alisema Bi Natai.
Ujenzi wa maghala na mapinduzi ya uhifadhi
Amesema,mojawapo ya hatua kubwa zilizochukuliwa ni ujenzi wa maghala ya kisasa katika ngazi ya halmashauri na vijiji. Maghala haya yamekuwa msaada mkubwa katika kupunguza upotevu wa mazao hasa ya nafaka, kutoka asilimia 30–40 hadi chini ya asilimia 20, huku lengo likiwa ni kufikia asilimia 5 tu katika siku za usoni.
“Tumekuwa tukitoa elimu kwa wakulima kuhusu njia sahihi za kuvuna, kukausha na kuhifadhi mazao ili kuepuka sumukuvu. Pia tunawahimiza wananchi kujenga maghala hata katika ngazi ya kaya,” aliongeza.
Sabasaba: Jukwaa la Elimu kwa Wakulima na Wananchi
Katika Maonyesho ya Sabasaba ya mwaka huu, Wizara ya Kilimo imejumuika na taasisi zake zaidi ya 21 ikiwemo Taasisi ya Utafiti wa Kilimo (TARI) ,Taasisi ya kudhibiti ubora wa Mbegu ( TOSC), Wakala wa Mbegu za Kilimo (ASA) , Mfuko wa Mbolea, Bodi ya Mazao Mchanganyiko, na nyingine nyingi zinazohusika moja kwa moja na maendeleo ya sekta ya kilimo.
Wakazi wa Dar es Salaam na wageni kutoka maeneo mbalimbali wamekuwa wakifurika katika banda la wizara hiyo wakipata elimu juu ya mbegu bora, matumizi sahihi ya zana za kilimo, teknolojia za umwagiliaji, na huduma za ugani.
“Kila mwaka tumekuwa tukijitosheleza kwa chakula kwa zaidi ya asilimia 100. Mwaka huu tumefikia asilimia 128 ya utoshelevu wa chakula kitaifa. Hii ni matokeo ya mipango thabiti ya serikali, hasa katika uwekezaji kwenye kilimo cha umwagiliaji, mbegu bora na huduma bora za ugani,” alisema Bi Natai.
Wizara inawahamasisha wananchi, wakulima na vijana kushiriki katika maonyesho haya ili kujifunza na kuwekeza zaidi katika kilimo chenye tija. Kupitia maonyesho haya, serikali inaamini itafanikisha lengo lake la kuwa na taifa lisilo na njaa, lishe bora na maendeleo ya kiuchumi yanayotokana na kilimo.

More Stories
Usajili wa Laini za Simu: Jilinde Dhidi ya Kutumiwa Vibaya kwa Utambulisho Wako
TTCL yaadhimisha siku ya Wanawake kwa kutoa msaada JKCI
Wananchi Dodoma washauri TBA kujenga nyumba za kupangisha watu binafsi