



Na Joyce Kasiki, TimesMajira Online – Maonyesho ya 49 ya Sabasaba, Dar es Salaam
MKURUGENZI Mkuu wa Taasisi ya Utafiti wa Kilimo Tanzania (TARI), ameeleza na taarifa njema kwa wakulima, wajasiriamali na wananchi kwa ujumla baada ya taasisi hiyo kuwasilisha teknolojia mbalimbali bunifu zitakazowawezesha kuongeza tija, kipato na thamani ya mazao katika maonyesho ya 49 ya Kimataifa ya Biashara ya Sabasaba yanayoendelea jijini Dar es Salaam.
Akizungumza na waandishi wa habari katika banda la TARI Julai 6,2025 , Mkurugenzi huyo alisema kuwa taasisi hiyo imejikita kuhakikisha teknolojia zinazozalishwa na taasisi hiyo zinatatua changamoto halisi zinazowakumba wakulima na kuongeza fursa kwa wafanyabiashara, wajasiriamali na jamii kwa ujumla.
“Wajibu wetu mkubwa ni kuhakikisha kuwa utafiti tunaoufanya hauishii kwenye machapisho ya kisayansi, bali unazalisha teknolojia zinazotumika na jamii kwa vitendo, kuongeza tija na hatimaye kipato,” alieleza.
Mashine ya Kupandia Mbegu (Rafiki Planter) Yabadilisha Mwelekeo wa Kilimo
Mojawapo ya teknolojia mpya iliyovutia wadau ni Rafiki Planter, mashine ya kupandia mbegu inayopunguza muda na gharama za upandaji wa pamba. Kawaida, hekta moja ya pamba huhitaji watu 10 hadi 16 kuipanda kwa saa nane. Kwa kutumia mashine hii, mtu mmoja pekee anaweza kupanda hekta moja kwa saa moja, hivyo kumuwezesha mkulima kuwahi mvua na kuongeza uzalishaji.
“Hii ni suluhisho la moja kwa moja kwa changamoto ya uhaba wa nguvu kazi na ucheleweshaji wa upandaji unaosababisha hasara,” alifafanua Mkurugenzi huyo.
Mabadiliko ya Nafasi za Upandaji Yazidisha Tija ya Pamba
TARI pia imefanya utafiti wa kina kuhusu nafasi za upandaji wa pamba, na kubaini kuwa nafasi mpya ya sentimita 60 kati ya mstari na 30 kati ya mche na mche imeongeza uzalishaji kutoka kilo 1,200 hadi 2,400 kwa hekta, huku baadhi ya wakulima wakiripoti kuvuna hadi kilo 2,700.
Mbegu Bora Za Migomba na Mihogo Zawavuta Wadau
Kwa upande wa migomba, TARI imezindua aina mbili bora za ndizi zinazozalisha hadi kilo 94 kwa mkungu mmoja ikilinganishwa na kilo 30 za aina ya kawaida. Aidha, kwa mihogo, mbegu ya TARICASS4 imeonyesha ongezeko la uzalishaji mara tano zaidi ya aina ya zamani.
Uongezaji Thamani: Mihogo, Karanga, Korosho na Nafaka
Katika jitihada za kuongeza thamani ya mazao, TARI imeonyesha bidhaa mbalimbali zinazotokana na mihogo kama tambi, biskuti, mkate na unga mbadala wa ngano. Aidha, taasisi hiyo imefanikiwa kubadilisha korosho zilizovunjika kuwa unga wa korosho unaotumika kutengeneza siagi na bidhaa nyingine zenye thamani kubwa.
Wajasiriamali pia wamehamasishwa kuchangamkia teknolojia ya kutengeneza juisi, divai na ethanol kutokana na mabibo ya korosho ambayo awali yalionekana kama taka.
Nafaka za Asili Zageuzwa Fursa
Kwa upande wa nafaka, TARI imeonesha matumizi mapya ya mtama, ulezi na uwele si tu kwa uji na ugali, bali pia kwa maandazi na bidhaa nyingine, sambamba na mbegu zinazostahimili magonjwa na wadudu.
“Lengo letu ni kuhakikisha kila mkulima au mjasiriamali anayefika kwenye banda letu anapata wazo la biashara au suluhisho la changamoto yake. TARI ni chimbuko la fursa na maendeleo,” alisisitiza Mkurugenzi Mkuu.
Taasisi hiyo imetoa wito kwa wananchi, wajasiriamali na makundi yote ya kijamii kutembelea banda lao ili kujifunza na kunufaika na teknolojia hizo, ambazo zinalenga kuongeza kipato na kuboresha maisha ya Mtanzania wa kawaida kupitia kilimo chenye tija na thamani.

More Stories
Usajili wa Laini za Simu: Jilinde Dhidi ya Kutumiwa Vibaya kwa Utambulisho Wako
TTCL yaadhimisha siku ya Wanawake kwa kutoa msaada JKCI
Wananchi Dodoma washauri TBA kujenga nyumba za kupangisha watu binafsi