March 7, 2026

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Njole:Sheria Zilizotafsiriwa kwa Kiswahili Kuanza Kutolewa Agosti

Na Joyce Kasiki, TimesMajira online

MWANDISHI Mkuu wa Sheria, Onorius Njole, amesema kuwa kuanzia mwezi Agosti mwaka huu, toleo la sheria zilizotafsiriwa kwa lugha ya Kiswahili litaanza kutolewa rasmi ili kuwawezesha wananchi wa makundi yote kuelewa na kufuata sheria kwa urahisi.

Akizungumza na waandishi wa habari Julai 7,2025 katika Maonesho ya 49 ya Kimataifa ya Biashara ya Sabasaba yanayoendelea jijini Dar es Salaam, Njole alisema agizo hilo lilitolewa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Samia Suluhu Hassan, kama sehemu ya maboresho ya mfumo wa sheria nchini.

“Pamoja na hatua kubwa ya urekebishaji wa sheria iliyofanyika, Rais aliagiza pia kukamilishwa kwa zoezi la kuzitafsiri sheria hizo kwa lugha ya Kiswahili ili ziweze kueleweka na wananchi wote,” alisema Njole.

Alieleza kuwa sambamba na mchakato wa kutafsiri sheria, Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali imeendelea kufanya mabadiliko makubwa ya kisheria ili kuhakikisha sheria zilizopo zinatekelezeka kwa ufanisi na kuwafikia wananchi kwa lugha rahisi na inayoeleweka.

“Tumefanya kazi ya kuboresha sheria ili zilingane na mahitaji ya sasa, lakini pia kuhakikisha zinapatikana kwa lugha ambayo wananchi wanaielewa vizuri – yaani Kiswahili,” aliongeza.

Aidha, Njole alisema kuwa ofisi yake imezikusanya sheria zote za nchi na kuzifanyia marekebisho ili kuondoa migongano ya vifungu na kurahisisha matumizi yake kwa wadau mbalimbali wa sheria na wananchi.

Katika hatua nyingine, Njole alibainisha kuwa serikali ipo katika mchakato wa kutengeneza mfumo wa kisheria kwa ajili ya kusimamia matumizi ya teknolojia ya Akili Mnemba (Artificial Intelligence – AI).

“Mfumo maalum kwa ajili ya kusimamia matumizi ya AI unaandaliwa na serikali. Mara baada ya kukamilika, miswada ya sheria itaandaliwa, na hatimaye kupitishwa kuwa sheria rasmi,” alisema.

Kwa upande wake, Mwandishi Msaidizi Mkuu wa Sheria, Bi. Rahema Katuga, alifafanua kuwa sheria zote zilizorekebishwa zimeanza kutumika rasmi kuanzia Julai 1, 2025. Alisema kuwa sheria za awali ambazo hazijafanyiwa marekebisho hazitatumika tena.

“Kuanzia sasa, katika vyombo vya sheria kama mahakama au sehemu nyingine yoyote ya utoaji haki, mtu atatakiwa kutaja vifungu vya sheria mpya vilivyoanza kutumika Julai mosi mwaka huu,” alieleza Katuga.