March 7, 2026

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Kilimo cha Mkonge ni fursa,Mkonge wa Tanzania wazidi kunga’ra kwa ubora Duniani

Na Joyce Kasiki, Timesmajira Online

KATIKA maonyesho ya 49 ya Kimataifa ya Biashara (Sabasaba), Bodi ya Mkonge Tanzania inahamasisha na kutoa elimu kwa wananchi kuhusu fursa lukuki zilizopo katika sekta ya mkonge, ikiwemo kilimo bora, uzalishaji wa mbegu na bidhaa zitokanazo na zao hilo.

Akizungumza katika banda la Bodi hiyo Julai 5,2025, Mkuu wa Sehemu ya Masoko na Uhamasishaji, David Magali, amesema kuwa lengo kuu la ushiriki wao katika maonyesho hayo ni kuhakikisha kuwa wanawafikia wadau wa sekta ya mkonge na kuwapatia elimu muhimu ili kuimarisha mnyororo mzima wa thamani wa zao hilo.

“Tunawaelimisha wakulima kuhakikisha wanazalisha mkonge unaokidhi viwango vya soko ndani na nje ya nchi. Hili ni zao lenye thamani kubwa na soko la uhakika,” amesema Magali.

Kwa mujibu wa Magali, Tanzania imebarikiwa kuwa na ardhi yenye rutuba inayofaa kwa kilimo cha mkonge, na ni muda muafaka kwa vijana na wawekezaji kujiunga na sekta hii yenye faida nyingi lakini yenye changamoto chache ikilinganishwa na mazao mengine.

Fursa zilizojaa thamani kwenye sekta ya Mkonge

Sekta ya mkonge inatoa fursa mbalimbali kwa Watanzania, ikiwemo kwenye uzalishaji wa Mbegu  kwani mahitaji ya mbegu ni makubwa kutokana na ongezeko la wakulima wanaochangamkia zao hili.

Ameitaja fursa nyingine ni uwekezaji katika Vituo vya Uchakataji ambapo amesema ,wakulima wengi wameshalima mkonge, hivyo kuna fursa kwa wawekezaji kuanzisha vituo vya kuchakata ili kuongeza thamani lakini pia amesema fursa nyingine ni utengenezaji wa Bidhaa za Mkonge .

“Tunavyo vituo Atamizi Tanga na Zanzibar hivyo tunakaribisha wabunifu na wakufunzi kuja kubuni bidhaa mbalimbali zitokanazo na mkonge kama vile mikoba, vikapu, mazulia na hata nyuzi za viwandani.

Tanzania yaongoza Duninia kwa ubora wa Mkonge

Afisa Kilimo Mwandamizi wa Bodi ya Mkonge Emanuel Lutego, amesema kuwa kwa sasa juhudi zinaelekezwa katika kuongeza uwezo wa uchakataji wa mkonge ili kufikia malengo ya kitaifa ya uzalishaji wa zaidi ya tani 120,000 kwa mwaka.

 “Kwa kuongeza mashine za kisasa za kuchakata, tutaongeza thamani ya mkonge wetu na kukuza uchumi wa wakulima. Tanzania inaongoza duniani kwa kuzalisha mkonge bora, na tunataka kuimarisha nafasi hiyo zaidi,” alisema Lutego.

Sekta ya mkonge nchini Tanzania siyo tu chanzo cha ajira na kipato, bali pia ni chachu ya maendeleo ya viwanda na ubunifu wa bidhaa. Bodi ya Mkonge inaendelea kuhimiza wananchi, hasa vijana na wawekezaji, kutumia fursa hii ya dhahabu kujiingiza katika kilimo, uchakataji na ubunifu wa bidhaa zitokanazo na mkonge.