Na Esther Macha,TimesmajiraOnline,Mbeya
MTANDAO wa Polisi Wanawake Mkoa wa Mbeya (TPF NeT) umetakiwa kujiweka vizuri katika kujifunza na kuelewa sheria mbalimbali ikiwemo za uchaguzi ili kutimiza majukumu yao kwa weledi.
Hayo yamesemwa na Mlezi wa Mtandao huo, Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mbeya Kamishna Msaidizi Mwandamizi wa Polisi (SACP) Benjamin Kuzaga Julai 4, 2025 wakati akifungua semina ya kuwajengea uwezo na uelewa wa masuala mbalimbali ya kiutendaji kazi, kijamii na kiuchumi Askari Wanawake wa Majeshi ya ulinzi na usalama mkoani humo.
Kamanda Kuzaga amesisitiza umuhimu wa Askari hao kushiriki kikamilifu kuimarisha ulinzi na usalama katika mchakato mzima wa uchaguzi, kabla, wakati na baada ili kuhakikisha uchaguzi unapita kwa amani na usalama.
“Semina hii pia itawajenga Askari Wanawake wa Jeshi la Polisi, JWTZ, Magereza, Zimamoto, Uhamiaji, Watumishi raia ndani ya Jeshi na Wake za Askari katika nyanja za kisheria, ujasiriamali na elimu ya afya ya akili ili kuwawezesha kutimiza majukumu yao kwa weledi na pia kujikwamia kiuchumi kupitia ujasiriamali”amesema Kamanda Kuzaga.
Kwa upande wake Mwenyekiti wa Mtandao wa Polisi Wanawake Mkoa wa Mbeya Mrakibu Mwandamizi wa Polisi (SSP) Salome Kabanje ameeleza kuwa dhumuni la TPF NeT Galla Party ni sherehe inayowakutanisha Askari Wanawake wa Majeshi yote, Wanawake Raia ndani ya Jeshi la Polisi na Wake za Askari ili kufahamiana na kupata elimu ya masuala mbalimbali.
Naye, Mwenyekiti wa Mtandao wa Askari Magereza Wanawake Mkoa wa Mbeya Mrakibu Mwandamizi wa Magereza (SSP) Deodata Timothy amelipongeza Jeshi la Polisi kupitia TPF NeT kwa kuwaunganisha Askari Wanawake wa majeshi yote ya ulinzi na usalama kwani kitendo hicho kinakusudia kuleta umoja, mshikamano na kudumisha upendo miongoni mwa Askari Wanawake katika utendaji kazi.
TPF NeT Galla hufanyika kila mwaka na uambatana na shughuli mbalimbali ikiwemo uwezeshaji wa kielimu, matendo ya huruma kwa kutembelea makundi yenye uhitaji na kujengeana uwezo na uelewa wa masuala mbalimbali ya kiutendaji kazi, kijamii, kiafya na kiuchumi.
Sherehe za TPF NeT, 2025 mkoani Mbeya zimebeba kauli mbinu inayosema, Nidhamu, Haki, Weledi na Uadilifu ni Msingi wa Mafanikio Yetu.



More Stories
Bilioni 7 kuwainua vijana 308 sekta ya uvuvi
Clara:Miaka 50 ya Sabasaba fursa mpya za Biashara na Uwekezaji
Usajili wa Laini za Simu: Jilinde Dhidi ya Kutumiwa Vibaya kwa Utambulisho Wako