
Tume kujenga uelewa kwa Umma kuhusu taratibu za malalamiko Mahakamani
Na Joyce Kasiki, TimesMajira Online
 MKUU wa Mawasiliano wa Tume ya Utumishi wa Mahakama, Lidya Churi, amesema kuwa Tume hiyo imejipanga kikamilifu kuwahudumia wananchi kwa kuwapatia elimu kuhusu namna ya kuwasilisha malalamiko yao dhidi ya maafisa Mahakama ili kuhakikisha haki inatendeka kwa wote.
Akizungumza na waandishi wa habari katika Maonyesho ya 49 ya Biashara ya Kimataifa ya Sabasaba yanayoendelea katika Viwanja vya Mwalimu Nyerere jijini Dar es Salaam, Churi amesema kuwa ushiriki wa Tume katika maonyesho hayo ni fursa muhimu kwao kutoa elimu kwa umma juu ya majukumu yake na namna ya kushughulikia malalamiko ya wananchi dhidi ya maafisa wa Mahakama.
 “Tume ya Utumishi wa Mahakama ni chombo cha kisheria kilichoanzishwa kwa mujibu wa Ibara ya 112(1) ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ya mwaka 1977, kikisomwa pamoja na Kifungu Na. 29(1) cha Sheria ya Usimamizi wa Mahakama Na. 237 ,tunayo dhamana kubwa ya kusimamia ajira na nidhamu za watumishi wa Mahakama, na ni muhimu wananchi waifahamu vyema Tume hii,” ameeleza Churi.
Ameongeza kuwa moja ya changamoto kubwa wanayokumbana nayo ni wananchi wengi kutofahamu majukumu ya Tume pamoja na Kamati zake za Maadili, jambo linalowakosesha fursa ya kuwasilisha malalamiko yao kwa njia sahihi.
Elimu kwa Umma, kiini cha Uwajibikaji
Churi alibainisha kuwa Tume hiyo ina jukumu la kumshauri Mheshimiwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kuhusu uteuzi wa Jaji Kiongozi, Majaji wa Mahakama Kuu, pamoja na uteuzi wa Mtendaji Mkuu wa Mahakama, Msajili wa Mahakama ya Rufani na Msajili wa Mahakama Kuu.
Mbali na hayo, Tume inawajibika kuchukua hatua za kiutawala na kinidhamu dhidi ya watumishi wa Mahakama katika mazingira ya ukiukwaji wa maadili, ikiwemo kuchunguza malalamiko dhidi ya Majaji na Mahakimu kupitia Kamati mbalimbali za Maadili.
Kamati hizo ni pamoja na Kamati ya Maadili ya Majaji, Kamati ya Maadili ya Maafisa wa Mahakama , na Kamati ya maadili ya Maafisa Mahakama ngazi ya Mkoa ,na Kamati maadili ya Maafisa Mahakama ngazi ya Wilaya.
“Majukumu ya Kamati hizi ni kupokea na kuchunguza malalamiko yaliyowasilishwa dhidi ya watumishi wa Mahakama, kuanzia ngazi ya Mahakama ya Rufani hadi Mahakama ya Mwanzo ambapo malalamiko hayo yanapaswa kuwasilishwa kwa maandishi, yakiwa na saini ya mlalamikaji na taarifa za kutosha kama vile maelezo ya tukio na mazingira yaliyohusika,” amesema Churi.
Ushirikiano na Wananchi Muhimu
Kwa mujibu wa Churi, Tume hiyo inahamasisha wananchi kushiriki kikamilifu kwa kutoa taarifa pale wanapohisi haki zao zimekiukwa au kuna ukiukwaji wa maadili wa maafisa wa Mahakama huku akisema taarifa hizo zinaweza kuhusisha tuhuma za rushwa, upendeleo, au uzembe katika kushughulikia kesi.
Hata hivyo, amesisitiza kuwa uwasilishaji wa malalamiko unapaswa kufuata taratibu na masharti ya kisheria ili kuwezesha uchunguzi kufanyika kwa ufanisi.
Changamoto na Mwelekeo wa Tume
Pamoja na jitihada hizo, Tume ya Utumishi wa Mahakama inakabiliwa na changamoto ya uelewa mdogo miongoni mwa wananchi kuhusu majukumu ya Tume na taratibu za kuwasilisha malalamiko. Hali hiyo, kwa mujibu wa Churi, hupelekea malalamiko kutofikishwa katika njia sahihi au kukosa vigezo vinavyotakiwa kisheria.
“Tunaendelea na juhudi za kutoa elimu ya mara kwa mara kwa umma ili kuhakikisha kila mwananchi anajua wapi na namna ya kuwasilisha malalamiko yake. Hii ni njia ya kuimarisha uwajibikaji na kurejesha imani ya wananchi kwa vyombo vya utoaji haki nchini,” alihitimisha.
Kwa sasa, Tume inaendelea kupokea wananchi katika banda lake kwenye maonyesho ya Sabasaba, ambapo inatoa elimu ya moja kwa moja kuhusu wajibu na utaratibu wa kuwasilisha malalamiko.

More Stories
Usajili wa Laini za Simu: Jilinde Dhidi ya Kutumiwa Vibaya kwa Utambulisho Wako
TTCL yaadhimisha siku ya Wanawake kwa kutoa msaada JKCI
Wananchi Dodoma washauri TBA kujenga nyumba za kupangisha watu binafsi