
Na Joyce Kasiki, Dar es Salaam
KAMISHNA Mkazi wa Tume ya Haki za Binadamu na Utawala Bora Zanzibar, Khatib Mwinyichande, amesema Tume hiyo ina nafasi ya kipekee na ya kikatiba katika kuhakikisha uchaguzi mkuu nchini unakuwa huru, haki na unaozingatia misingi ya utawala bora.
Akizungumza na waandishi wa habari katika Maonyesho ya 49 ya Biashara ya Kimataifa ya Dar es Salaam (Sabasaba), kwenye banda la Tume hiyo, Mwinyichande alibainisha kuwa jukumu kubwa la Tume ni kulinda na kuhifadhi haki za binadamu pamoja na misingi ya utawala bora, jambo linaloifanya kuwa na nafasi ya moja kwa moja katika mchakato wa uchaguzi.
“Uchaguzi si tukio la kisiasa pekee, bali ni jambo linalogusa haki za msingi za wananchi,kwa kuwa nchi yetu ni ya kidemokrasia, viongozi hupatikana kupitia uchaguzi huru na wa haki ,na hilo ndilo jukumu kuu la Tume yetu…,kuhakikisha misingi ya kisheria na haki za binadamu zinalindwa katika kila hatua ya uchaguzi,” alisema.
Kamishna huyo alisema Tume ya Haki za Binadamu itakuwa miongoni mwa waangalizi wa uchaguzi kuanzia kampeni, hadi siku ya kupiga kura, huku akisisitiza kuwa Tume itakuwa ikifuatilia mwenendo wa uchaguzi na kuandika ripoti itakayowasilishwa kwa mamlaka husika.
“Katika kila hatua ya uchaguzi, Tume inachunguza, inabaini changamoto au mapungufu, na kuyawasilisha kwa mamlaka ya uchaguzi kwa ajili ya marekebisho kwenye uchaguzi unaofuata. Hii ni njia mojawapo ya kulinda haki za wananchi,” aliongeza.
Kuhusu Maonyesho ya Sabasaba
Akizungumzia ushiriki wa Tume hiyo kwenye Maonyesho ya Sabasaba, Mwinyichande alisema ni sehemu ya kutekeleza jukumu lake la kuelimisha umma kuhusu haki, wajibu na namna ya kuishi kwa kuheshimu sheria na misingi ya demokrasia.
“Maonyesho haya yanatuwezesha kukutana moja kwa moja na wananchi, kupokea malalamiko yao, kutoa elimu ya haki za binadamu, na kuwaeleza kuwa sisi ni watetezi wao pale wanapokwazwa na kukosa haki zao,” alisema Kamishna.
Alisisitiza kuwa elimu hiyo inawasaidia wananchi kufahamu kuwa haki zao zinalindwa kisheria, na kwamba Tume ipo kwa ajili ya kuhakikisha kuwa hakuna mwananchi anayebaguliwa au kunyimwa haki zake kwa misingi yoyote.
Maonyesho ya Sabasaba yamekuwa yakitumika na taasisi mbalimbali kama jukwaa la kuwasiliana moja kwa moja na wananchi. Tume ya Haki za Binadamu na Utawala Bora inatumia fursa hiyo kuimarisha uelewa wa umma kuhusu haki za msingi, utawala bora na njia sahihi za kudai haki .

More Stories
Usajili wa Laini za Simu: Jilinde Dhidi ya Kutumiwa Vibaya kwa Utambulisho Wako
TTCL yaadhimisha siku ya Wanawake kwa kutoa msaada JKCI
Wananchi Dodoma washauri TBA kujenga nyumba za kupangisha watu binafsi