March 7, 2026

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Maonyesho ya 49 ya Sabasaba,Wizara ya Katiba na Sheria Yatoa Elimu ya Haki na Wajibu kwa Wananchi

Na Joyce Kasiki, TimesMajira Online – Dar es Salaam

WIZARA   ya Katiba na Sheria kupitia Kitengo cha Katiba na Ufuatiliaji Haki imeendelea kutoa elimu kwa wananchi juu ya masuala ya utawala bora, haki za binadamu, wajibu wa kiraia na mifumo ya utoaji haki nchini.

Akizungumza katika banda la wizara hiyo katika Maonyesho ya 49 ya Kimataifa ya Biashara ya Sabasaba yanayoendelea jijini Dar es Salaam,Wakili wa Serikali kutoka Wizara ya Katiba na Sheria,  Doris Ndalio, amesema kuwa kitengo hicho kimejikita katika kutoa uelewa kwa wananchi kuhusu haki zao za msingi na wajibu wao kama raia wa Tanzania, sambamba na kutoa mwongozo juu ya namna ya kufuatilia haki zao kupitia mifumo rasmi ya kisheria.

“Tunatoa elimu kuhusu masuala yanayohusiana na Katiba, utawala bora, demokrasia, uraia na wajibu wa kila Mtanzania, ikiwemo kutekeleza jukumu la ulinzi wa nchi yetu. Lakini pia tunapokea na kufanyia kazi malalamiko kutoka kwa wananchi waliokosa haki, na kuyafikishia mamlaka husika,” ameema Ndalio.

Kwa mujibu wa maelezo yake, Kitengo cha Katiba na Ufuatiliaji Haki kimekuwa daraja muhimu kati ya wananchi na taasisi mbalimbali za utoaji haki, kama Mahakama, Tume ya Haki za Binadamu na Utawala Bora, pamoja na vyombo vingine vya kisheria.

Huduma kwa wateja yapongezwa

Akitembelea banda hilo, Kamishna wa Tume ya Haki za Binadamu na Utawala Bora, Dkt. Thomas Masanja, amepongeza huduma zinazotolewa na wizara kupitia kitengo cha huduma kwa mteja, akieleza kuwa mfumo wa kupokea na kufuatilia malalamiko umejengwa kwa weledi na uwazi.

“Nimevutiwa na mfumo wao wa kushughulikia malalamiko hata yale yasiyohusu moja kwa moja wizara yao na kuhakikisha yanapatiwa ufumbuzi. Ni jambo jema, na sisi kama Tume tumejifunza mengi, tutarejea kwa ajili ya kuongeza ufanisi wetu pia,” amesema Dkt. Masanja.

Wito Katika Kipindi cha Uchaguzi

Ndalio amesema katika kipindi hiki kuelekea uchaguzi, wizara imejielekeza pia kuhimiza wananchi kutimiza haki yao ya kikatiba kwa kujiandikisha, kupiga kura na hata kuomba kugombea nafasi za uongozi, akisisitiza kuwa haki hizo ni msingi wa demokrasia na utawala bora nchini.

“Ni muhimu wananchi wafahamu kuwa kushiriki kwenye uchaguzi ni haki ya msingi, lakini pia ni wajibu wa kiraia. Tunalenga kuwaelimisha zaidi kuhusu hili katika kipindi hiki muhimu,” ameongeza.

Kamishna huyo pia amepongeza Kampeni ya Kisheria ya Mama Samia, ambayo imekuwa ikitoa msaada wa kisheria bure kwa wananchi, akieleza kuwa imeleta tija kubwa kwa jamii hasa katika mikoa 26 iliyofikiwa awamu ya kwanza.

Ameshauri kampeni hiyo iendelezwe zaidi kwa awamu nyingine, hasa katika maeneo yaliyoonekana kuwa na uhitaji mkubwa wa huduma za msaada wa kisheria.

Kwa ujumla, ushiriki wa Wizara ya Katiba na Sheria katika maonyesho ya Sabasaba mwaka huu unaendelea kuwa jukwaa muhimu la kutoa elimu ya kisheria, kuhamasisha usawa wa haki, na kukuza utawala bora nchini.