Na Yusuph Mussa,Timesmajiraonline,Lushoto
MMOJA wa watia nia ndani ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) Dkt. Wemael Chamshama anatarajia kupambana na ‘vigogo’ katika kutafuta ridhaa ya kupeperusha bendera ya chama hicho Jimbo la Lushoto mkoani Tanga kwenye Uchaguzi Mkuu mwaka huu.
Dkt.Chamshama ameungana na waomba ridhaa hao baada ya kuchukua fomu Julai Mosi, 2025 kwenye Ofisi ya CCM Wilaya ya Lushoto na kuweza kuungana na aliyekuwa Katibu Mkuu Wizara ya Mifugo na Uvuvi Profesa Riziki Shemdoe, aliyekuwa Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Lushoto, Mathew Mbaruku na Mbunge wa sasa Jimbo la Lushoto, Shaaban Shekilindi.

Dkt. Chamshama ambaye ana Shahada ya Uzamivu (PhD) ya Elimu aliyoipata nchini Sierra Leone, Shahada ya Uzamili (Masters) ya Elimu na Shahada ya Kwanza ya Elimu katika Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, alianza kazi Baraza la Mitihani Tanzania (NECTA) mwaka 2008- 2018, na tangu 2018, yupo Halmashauri ya Jiji la Dar es Salaam, Idara ya Elimu Sekondari kama Afisa Taaluma Mwandamizi.
Kwenye masuala ya siasa, mwaka 2005 alijiunga CCM, na mwaka 2020 aligombea ubunge Viti Maalum Mkoa wa Tanga wakati mwaka 2022 aliteuliwa kugombea Uwenyekiti UWT Taifa, kuteuliwa kugombea Umakamu Mwenyekiti Wazazi Taifa, na kuomba kugombea Ubunge Africa Mashariki. Mwaka 2023 aliteuliwa kuwa Mjumbe Kamati ya Elimu Malezi Wazazi Taifa.

Mwingine aliyechukua fomu Jimbo la Lushoto ni Wakili msomi Remigius Mainde, na Mkurugenzi wa kampuni ya RFA International Attorneys, kada na wakili wa Chama Cha Mapinduzi Mkoa wa Mwanza. Amesoma Chuo Kikuu cha Mtakatifu Augustino jijini Mwanza LLB na Post graduate Diploma in legal Practice (PGDLP) ( law school) Dar es salaam.
Hussein Mshangama ambaye anawania ubunge Jimbo la Bumbuli ni mtaalamu mwenye weledi katika masuala ya Financial Inclusion, Mikopo ya Biashara (Business Lending) na mikopo ya mashirika (corporate lending), akiwa na Shahada ya Kwanza ya fedha na benki kutoka Chuo Kikuu cha Dar es Salaam. Uzoefu wake katika uongozi unajumuisha nyadhifa kama Katibu wa Uchumi na Fedha wa CCM Chuo cha UDSM na Mbunge wa DARUSO kati ya mwaka 2015 hadi 2017.

Mwingine ni Afisa Habari wa Dayosisi ya Kaskazini Mashariki ya Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT) Hellen Mushi ambaye amechukua fomu ya kuwania ubunge Jimbo la Lushoto.
Naye Joe Vyankero anawania udiwani Kata ya Lushoto. Ni kijana mwenye maono makubwa ya kuibadilisha Lushoto na kuonekana kama inavyotambulika kimataifa, ambapo amefanikiwa kuandaa matamasha makubwa ya kiserikali kama Mwenge wa Uhuru 2023 2024 kama mwana Kamati, na Usambara Tourism Festival ambayo ilisimamiwa na Ofisi ya Mkuu wa Wilaya ya Lushoto, na matamasha ya taasisi za maendeleo Wilaya ya Lushoto kama Usambara Festival ambayo imempa nafasi kubwa ya kuwaunganisha wananchi na viongozi wa Serikali pamoja.


“Dkt. Wemael Chamshama.”


More Stories
Wanawake washauriwa kuchangamkia fursa za uchumi
Aida:Wanawake wakipata haki zote itapunguza migogoro
LGTI wanawake waadhimisha siku yao Ngorongoro