
Na Joyce Kasiki, TimesMajira Online,Dar es Salaam,
MKUU wa Matawi na Mauzo wa Benki ya NMB Donatus Richard, amesema benki hiyo ipo imara kuwahudumia Watanzania katika maonesho ya 48 ya Biashara ya Kimataifa ya Dar es Salaam (Sabasaba), ikiambatana na huduma bora, teknolojia mpya na mikakati ya kisasa ya kuwawezesha wateja wake, hususani wafanyabiashara na wakulima.
Akizungumza na waandishi wa habari,leo Juni 30,2025 katika viwanja vya Sabasaba kwenye banda la.benki hiyo , Donatus amesema “Tupo hapa kuwahudumia Watanzania kwa karibu,tunatoa huduma za bima, huduma za kilimo biashara, pamoja na kufungua akaunti kuanzia watoto mpaka watu wazima.”amesema Richard
Aidha amesema,mbali na tawi letu lililopo katika viwanja vya sabasaba kwa ajili ya kutoa huduma,pia wamesambaza mawakala wa NMB kila kona ili wananchi waweze kuhudumiwa kirahisi kwa huduma wanataka iwe ni kuweka au kutoa pesa, au kupata huduma nyingine mbalimbali za kibenki.
Amesema,MMB inatarajia kuhudumia zaidi ya wafanyabiashara 3,000 na kupokea wateja zaidi ya 900,000 katika kipindi chote cha maonesho ya Sabasaba mwaka huu.
“Kwa wale wafanyabiashara ambao bado hawana akaunti, huu ni wakati sahihi ,tupo hapa kwa ajili yao. Pia, tumeweka dirisha maalum kwa ajili ya ulipaji wa ada na kodi mbalimbali za serikali kama vile malipo ya vitambulisho vya Taifa (NIDA), Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA ) na mengineyo,” ameongeza Donatus.
Kwa mujibu wa Richard,kwa kaulimbiu ya mwaka huu inayolenga kuwa karibu na wateja, NMB imedhihirisha dhamira hiyo kwa kuhakikisha watalaam wake wa mikopo, kilimo, na fedha wapo tayari kutoa ushauri na msaada wa moja kwa moja kwa wote wanaotembelea maonesho hayo.
“Kwa wale wanaotaka mikopo, hasa wafanyakazi, tumewaletea watalaam wetu ambao watakuongoza hatua kwa hatua jinsi ya kuomba mkopo kupitia benki yako ya NMB,kwa wakulima, tuna akaunti maalum na mikopo yenye masharti nafuu inayotolewa kwa haraka,” amesema.
Akizungumza kuhusu huduma za kidigitali amesema, NMB imekuja kivingine mwaka huu kwa kuzindua mashine mpya za kuweka pesa zilizopo katika maeneo mbalimbali kama Mlimani City, Mbagala, Mwanjelwa, Bahamas, Rock City, na Kariakoo.
Mashine hizi kwa sasa zimefikia 11, na benki inaendelea kupanua wigo huo katika maeneo mengine ili kuongeza urahisi wa kupata huduma bila kufika matawini.
Aidha amesema NMB imeongeza kiwango cha huduma kwa njia ya simu ambapo sasa mteja anaweza kutuma au kutoa hadi milioni 30 kupitia simu, kutoka kiwango cha awali cha milioni tano.
Pia, uwezo wa kutuma pesa nje ya nchi kama Kenya, Rwanda, Afrika Kusini na nchi nyingine unaboreshwa kwa kasi, huku wateja wakipewa uwezo wa kujisajili wenyewe kwa kutumia simu zao.

More Stories
Bilioni 7 kuwainua vijana 308 sekta ya uvuvi
Clara:Miaka 50 ya Sabasaba fursa mpya za Biashara na Uwekezaji
Usajili wa Laini za Simu: Jilinde Dhidi ya Kutumiwa Vibaya kwa Utambulisho Wako