- Kunufaisha zaidi ya wakazi 14,000 Wilaya ya Kondoa
Na Mwandishi Wetu, TimesMajira Online



KAMPUNI ya Bia ya Serengeti (SBL), kwa kushirikiana na shirika la Africa Community Advancement Initiative (Africai), imezindua rasmi Mradi wa Maji wa Kwadelo katika Wilaya ya Kondoa, Mkoa wa Dodoma. Mradi huu unatarajiwa kuwanufaisha zaidi ya wakazi 14,750 wa Kata ya Kwadelo kwa kuwapatia maji safi na salama kila siku.
Mradi huu uliozinduliwa na Waziri wa Mifugo na Uvuvi na Mbunge wa Jimbo la Kondoa, Dkt. Ashatu Kijaji, umegharimu zaidi ya shilingi milioni 292, ukiwa ni sehemu ya jitihada za SBL kusaidia jamii kupitia programu yao ya muda mrefu ijulikanayo kama Water of Life.
Kwa mujibu wa taarifa iliyosambazwa kwa wanahabari, Mradi wa Kwadelo umehusisha, ufungaji wa pampu ya kuvuta maji ya kisasa (submersible pump), ujenzi wa nyumba ya mashine na tanki la kuhifadhi maji la saruji na uwekaji wa mtandao wa mabomba ya kusambaza maji kwa umbali mkubwa.

Aidha mradi huo pia umehushisha ujenzi wa vituo 11 vya kuchotea maji vinavyoweza kuzalisha zaidi ya lita 107,000 za maji kwa siku.
“Maji ni uhai,” alisema Mkurugenzi Mtendaji wa SBL, Obinna Anyalebechi, akibainisha kuwa upatikanaji wa maji salama ni msingi wa maendeleo ya kijamii na kiuchumi.
Katika hotuba yake, Dkt. Kijaji alipongeza ushirikiano wa SBL na serikali, akisema,
“Maji siyo tu hitaji la msingi, bali ni heshima, afya, na fursa kwa jamii. Tunahitaji mashirika kama SBL katika safari yetu ya kuleta mabadiliko ya kijamii vijijini.”
Mradi wa Kwadelo unajengwa kama mfano wa mafanikio ya ushirikiano wa sekta binafsi na serikali katika kutatua changamoto za msingi kama maji safi, hasa kwa maeneo ya pembezoni.


Tangu mwaka 2010, SBL imeanzisha zaidi ya miradi 28 ya maji nchini Tanzania, ikiwa ni msaada kwa zaidi ya Watanzania milioni 2. Kila mradi unalenga kuongeza upatikanaji wa huduma za maji safi na kuchochea maendeleo ya afya, elimu, na uchumi vijijini.
Kupitia dira yake ya ESG (Mazingira, Jamii na Utawala Bora), pamoja na mwelekeo wa Maendeleo ya Taifa 2050, SBL imejipambanua kama mdau muhimu wa maendeleo jumuishi nchini Tanzania.
SBL imetoa wito kwa mashirika mengine ya maendeleo, taasisi za serikali na sekta binafsi kuungana pamoja katika kuwekeza kwenye miradi ya maji na huduma muhimu za kijamii ambazo zinabadilisha maisha ya Watanzania.





More Stories
TUCASA yaomba kuanzishwa sheria malipo sekta ya ujenzi
Kihongosi:Uhai wa chama mashina
Kihongosi: Msigombane kwa itikadi za vyama