March 7, 2026

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Vijana CCM Dar,watoa wito watanzania kujitokeza kushiriki uchaguzi Oktoba,2025

Na Mwandishi wetu,TimesmajiraOnline,Dar

VIJANA wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Mkoa wa Dar es salaam wametoa Wito kwa watanzania kujitokeza kwa wingi na  kushiriki kwenye uchaguzi Mkuu unaotarajia kufanyika Oktoba mwaka huu kwa Amani na utulivu .

Wito huo umetolewa jijini hapa wakati wakizungumza na waandishi wa habari kuhusu masuala mbalimbali ikiwemo ushiriki wa vijana katika uchaguzi Mkuu Kwa mwaka 2025 na kutoa ufafanuzi wa Sheria za uchaguzi.

Wamesema Oktoba mwaka huu kutafanyika jambo la kikatiba ambalo linaelekeza watanzania wote kushiriki katika uchaguzi.

Mabula Marco ni miongoni mwa vijana hao aliwaomba vijana kujitokeza kwa wingi kuchukua fomu wa ajili ya kugombea nafasi mbalimbali pamoja na kushiriki kikamilifu kuwachagua viongozi.

“Nawaomba Vijana wezangu mjitokeze kwa wingi kuchukua fomu za kugombea nafasi za Udiwani na Ubunge pamoja na kumpigia kura Mgombea urais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania(CCM),Dkt.Samia Suluhu Hassan,”amesema Marco.

Aidha amekipongeza Chama cha Mapinduzi (CCM) kwa kuweka utaratibu mzuri wa kuhakikisha kila kijana mwenye uwezo na sifa za kuongoza Taifa hili anashinda .

Kwa upande wake Isack Sumbali ambaye naye ni miongoni mwa vijana hao alisema mabadiliko ya Sheria ya Uchaguzi yamefanyika kwa kiasi kikubwa ikiwemo Tume ya Taifa ya Uchaguzi(NEC) kubadilishwa na kuwa Tume huru ya Taifa ya  Uchaguzi(INEC).

Hivyo alitoa wito kwa watanzania kujitokeza kuwania nafasi mbalimbali ambazo zitatagazwa na Tume hiyo.

“Uchaguzi Mkuu unaotarajia kufanyika Oktoba mwaka huu upo palepale na hakuna umma wowote unaoweza kuzuia uchaguzi usifanyike kwani uchaguzi upo kikatiba, “alisisitiza.

Aidha aliwaonya wanaharakati,wanasiasa wanaopotosha wananchi wasishiriki Uchaguzi Mkuu  kwa madai kuwa hakuna mabadiliko yaliyofanywa kwenye Sheria za Uchaguzi.

“Atutakubali kuona watu wanaingia barabarani kuzuia uchaguzi na badala yake tutawapatia elimu ili washiriki uchaguzi Mkuu”amesema

Kwa upande wake  Antipas Pamba amesema kwamba takwimu za Sensa ya Watu na Makazi zinaonesha asilimia 70 ya wakazi Nchini Tanzania ni Vijana hivyo kila jambo ambalo Serikali inalitekeleza wanufaika wakubwa wa jambo hilo ni Vijana.

Amesema kuwa Serikali imeendelea kutoa Mikopo kwa wanafunzi wa Elimu ya Juu na Vyuo vya kati,hadi sasa kiasi cha shilingi trilioni 2.7 zimetumika katika mpango huo wa kusomesha watoto wenye hali ya maisha ya chini,pamoja na kutumia kiasi cha shilingi bilioni 709 kwa ajili ya kutoa ruzuku ya mbolea kwa Wakulima.