March 7, 2026

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Balozi Nchimbi: Maoni kuhusu amani ya nchi hayajawahi kupuuzwa

Na Agnes Alcardo, Timesmajira Online.

KATIBU Mkuu wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Balozi Dkt. Emmanuel Nchimbi, amesema, maoni yoyote yanayolenga kuendelea kudumisha amani na utulivu wa nchi, hayajawahi kupuuzwa na hayatapuuzwa.

Pia Balozi Nchimbi, amesema Mwenyekiti wa CCM na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan, ni mwanamke ambaye uongozi wake umeongeza heshima kwa wanawake na Tanzania.

Akiendeleza safari iliyoanzishwa na viongozi wengine wanawake jasiri, tangu wakati wa kudai uhuru na kuiweka Tanzania katika ramani ya dunia.

Balozi Dkt. Nchimbi amesema hayo wakati akifungua Jukwaa la Wanawake wa Arusha 2025, lililokuwa na mada ya ‘Safari ya Mwanamke Arusha 2025′,lililofanyika katika ukumbi wa mikutano wa Kimataifa wa Arusha (AICC), jijini Arusha, Juni 24, 2025.

“Hivyo ndivyo wanawake wanalitazama taifa letu (kama wanavyotazama watoto wao). Wanataka nchi yetu iendelee kuwa na amani, nchi yetu iendelee kuwa tulivu. Nataka nitumie nafasi hii, kuwahakikishia wanawake wa Tanzania, kwamba CCM inatambua dhamana yake ya kulinda amani ya nchi yetu,”.

“Nataka niwahakikishie viongozi wa mila,dini na taasisi za kijamii pamoja na Watanzania wote, kwamba maoni yenu yanayohusu kuendeleza amani na utulivu katika nchi yetu, hatujawahi kuyapuuza kama Chama Cha Mapinduzi,”amesema Balozi Nchimbi na kuongeza;

“Tunatambua kuwa amani ndiyo kipaumbele cha kwanza cha mwanamke wa Tanzania,akitambua kwamba kuilinda amani ni kuilinda nchi yetu, kukilinda kizazi cha sasa na kizazi kijacho, tutaendelea kuisimamia amani ya nchi yetu kwa nguvu zetu zote,”.

Jukwaa hilo ambalo wazungumzaji wakuu wa mada hiyo walikuwa ni pamoja na Mama Fatma Karume, mjane wa Hayati Mzee Abeid Amani Karume, Mama Anne Makinda, Dkt. Asha-rose Migiro, Zakhia Meghji, na wanawake wengine vijana, lililenga kuzungumzia safari ya mwanamke katika nyanja mbalimbali za maisha, kisiasa, kiuchumi na kijamii nchini.