
Skanka yazidi kusambaa: Ongezeko Kubwa la Dawa za Kulevya tishi kwa vijana
Na Joyce Kasiki, Dodoma
WAZIRI wa Nchi,Ofisi ya Waziri ,Mkuu,Sera,Bunge na Uratibu William Lukuvi amesema,matumizi ya dawa ya kulevya aina ya skanka yameongezeka kwa kiwango cha juu cha kemikali ya THC hali ambayo ni tishio kwa vijana ambao ni nguvu kazi ya Taifa.
Akizungumza jijini Dodoma na waandishi wa habari leo Juni 23,2025, kuhusu taarifa ya hali ya dawa za kulevya kwa mwaka 2024, Lukuvi alisema,kilevi hicho kinazidi kupata umaarufu miongoni mwa vijana nchini .
Akitoa taarifa hiyo ,alisema ripoti mpya ya Mamlaka ya Kudhibiti na Kupambana na Dawa za Kulevya inaonesha kuwa kiasi cha Skanka kilichokamatwa mwaka huu kimeongezeka kwa asilimia 89.8 ikilinganishwa na mwaka jana.
“Ishara ya changamoto kubwa inayoendelea kuikumba nchi katika mapambano dhidi ya dawa hizo haramu.”alisema Lukuvi
Kwa mujibu wa ripoti hiyo, jumla ya tani 2,307.37 za bangi zilikamatwa mwaka huu, ambapo tani 4.17 kati ya hizo ni Skanka iliyoingizwa nchini kutoka nchi za Kusini mwa Afrika.
“Hili linaonesha jinsi biashara ya dawa za kulevya inavyozidi kuimarika kimataifa, ikivuka mipaka na kuingia Tanzania kupitia njia za kisasa na zisizo rasmi.”
Alisema,wakati Skanka ikionesha kuongezeka kwa kasi, dawa nyingine zinazotokana na mimea kama mirungi zimeendelea kuwepo kwa wingi nchini, ambapo jumla ya tani 18.45 za mirungi zilikamatwa katika operesheni mbalimbali.
“Hili linaashiria kwamba dawa za kulevya zinazopatikana kwa urahisi vijijini bado ni tatizo sugu linalohitaji juhudi za pamoja kulidhibiti.”alisisitiza
Kwa upande wa dawa za kulevya zinazozalishwa viwandani, alisema mafanikio makubwa yamepatikana ambapo Serikali imefanikiwa kukamata tani 1.7 za methamphetamine, kilogramu 433.02 za heroin na gramu 853 za cocaine.
Kwa mara ya kwanza, dawa mpya ya kulevya aina ya MDPV nayo ilikamatwa ikiwa na uzito wa kilo tano, hatua inayodhihirisha namna wauzaji wa dawa hizi wanavyobadili mbinu kila mara.
Vile vile alisema,jitihada za kudhibiti kemikali bashirifu na dawa tiba zenye asili ya kulevya pia zimeimarishwa kwa kiasi kikubwa. Kwa mwaka huu pekee, kilo 19.2 na lita 22,682.4 za kemikali hizo zilikamatwa, huku mifumo ya kielektroniki ikisaidia kuzuia uingizwaji wa tani 29.6 na lita 125 za kemikali bashirifu kabla hazijafika sokoni.
Katika upande wa tiba na msaada wa kijamii, alisema Serikali imeendelea kutoa huduma za methadone kwa waraibu wa heroin kupitia vituo 16 vilivyofanikisha kusajili waraibu 17,975. Pia, nyumba 62 za upataji nafuu (sober housaes) zimewasaidia waraibu 17,230 wa dawa mbalimbali kurejea katika maisha ya kawaida.
“Kwa mafanikio haya, Serikali inatoa shukrani kwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa dhamira yake ya dhati katika kupambana na janga hili,Mamlaka ya Kudhibiti na Kupambana na Dawa za Kulevya, vyombo vya usalama, wataalamu wa afya na wadau mbalimbali wamechangia pakubwa katika mafanikio haya.”
Pamoja na hatua hizi, Serikali inasisitiza kuwa mapambano dhidi ya dawa za kulevya hayawezi kufanikiwa kwa juhudi za mtu mmoja au taasisi moja huku ikisema kuwa ,hili ni tatizo linalohitaji mshikamano wa kitaifa kutoka kwa jamii, familia, mashirika ya kiraia na sekta binafsi.
Amewahimiza wananchi kutoa taarifa pale wanapobaini uwepo wa biashara au matumizi ya dawa za kulevya ambapo alisema, kupitia ushirikiano huo wa karibu kati ya Serikali na wananchi ndipo Tanzania inaweza kufanikisha dhamira yake ya kuwa Taifa huru dhidi ya matumizi na biashara ya dawa za kulevya.
Kwa upande wake Kamishna wa Dawa za kulevya nchini Lyimo amesema yeyote anayehamasisha matumizi ya dawa za kulevya kwa namna yoyote ile anakiuka taratibu na atachukuliwa Sheria Kali.
“Kwa mujibu wa Sheria ya kudhibi na kupambana na dawa za kulevya inakatza kubwa mavazi au kuhamasisha kwa namna yoyote iwe mavazi ,nyimbo au njia yoyote ile ,ukikutwa na hatia basi unafungwa gerezani.”amesema Lyimo
Aidha kuhusu shisha amesema,hiyo siyo dawa za kulevya isipokuwa wapo baadhi ya watu Wasio waaminifu ambao wamekuwa wakichukua dawa za kulevya na kuongeza kwenye shisha mwisho wa siku Watumiaji wa shisha ,wanakuwa waraibu wa Dawa hizo na kuwa wagonjwa.
“Kwa hiyo sasa hivi Sheria inatungwa kuhusiana na suala hilo na tayari linafanyiwa kazi na lipo kwenye hatua ya kuchukua maoni ya wananchi Ili kuona namna ya kudhibiti shisha Ili watu Wasio waaminifu wasiweze kunitumia kuweka dawa za kulevya kwenye shisha na kuvutia watu kuanza matumizi ya dawa hizo.”

More Stories
Usajili wa Laini za Simu: Jilinde Dhidi ya Kutumiwa Vibaya kwa Utambulisho Wako
TTCL yaadhimisha siku ya Wanawake kwa kutoa msaada JKCI
Wananchi Dodoma washauri TBA kujenga nyumba za kupangisha watu binafsi