March 7, 2026

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Waziri Mkuu Majaliwa afunga rasmi Bunge Bonanza

Na Joyce Kasiki,Timesmajira online, Dodoma

Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Kassim Majaliwa, ameongoza mamia ya wabunge, viongozi wa serikali, wadau wa maendeleo na wananchi wa jiji la Dodoma katika kufunga rasmi Bonanza Maalum la Bunge – Grand Bunge Bonanza – lililofanyika kwa kishindo katika uwanja wa shule ya msingi John Mellin jijini Dodoma, ikiwa ni bonanza la mwisho kwa Bunge la 12.

Katika hotuba yake ya kufunga bonanza Hilo la kihistoria Leo Juni 21,2025, Waziri Mkuu Majaliwa alisisitiza kuwa michezo ni zaidi ya burudani; ni jukwaa la kudumisha afya, mshikamano na ustawi wa jamii. Alieleza kuwa Serikali itaendelea kuunga mkono jitihada za Bunge katika kutumia michezo kama nyenzo ya kuimarisha umoja wa kitaifa.

> “Kwa miaka mitano mfululizo, Grand Bunge Bonanza limekuwa ni jukwaa la kuhamasisha mazoezi, afya bora na mshikamano wa kitaifa. Faida zake zimegusa nyanja nyingi kuanzia kwa wabunge, wafanyakazi wa Bunge hadi kwa wananchi wa kawaida,” alisema Majaliwa.

Bonanza hilo limejumuisha michezo mbalimbali ikiwemo mpira wa miguu, netiboli, kuvuta kamba na riadha, likibeba kaulimbiu yenye uzito wa kijamii: “Michezo kwa Afya, Umoja na Maendeleo.”

Naibu Spika wa Bunge, Mussa Zungu, naye alipongeza ushiriki wa wadau mbalimbali wakiwemo sekta binafsi kama Benki ya CRDB, huku akilitaja kwa mfano wa kuigwa mchango wa benki hiyo katika elimu – ukiwemo ujenzi wa shule ya kisasa katika Wilaya ya Ilala.

Kwa upande wake Mwenyekiti wa Bonanza hilo ambaye pia ni Mbunge wa Makete, Festo Sanga, alieleza kuwa tukio hilo limekuwa chachu ya mshikamano, afya ya mwili na akili pamoja na kujenga urafiki na ushirikiano baina ya wabunge, taasisi za serikali, sekta binafsi na wananchi kwa ujumla.

> “Michezo ni zaidi ya burudani; ni daraja la kuunganisha jamii, kukuza vipaji na hata kutoa fursa za ajira kwa vijana wetu,” alisisitiza Sanga.

Katika kuunga mkono wiki ya kuzuia matumizi ya dawa za kulevya, Kamishna Jenerali wa Mamlaka ya Kudhibiti Dawa za Kulevya, Aretas James Lyimo, alitumia jukwaa hilo kutoa salamu maalum, akieleza kuwa michezo ni njia mojawapo ya kumkinga kijana na janga la dawa hizo hatari.

> “Bonanza hili limekuja wakati mwafaka ambapo tunahamasisha jamii juu ya hatari za dawa za kulevya. Michezo hutoa mbadala chanya kwa vijana na ni njia bora ya kujenga taifa lenye afya na nidhamu,” alisema Lyimo.

Vilevile, Kamishna Lyimo alitoa wito kwa Watanzania wote kushiriki kikamilifu katika uchaguzi mkuu unaotarajiwa kufanyika mwezi Oktoba, akisisitiza umuhimu wa ushiriki wa wananchi katika ujenzi wa demokrasia.

Kwa upande wake, Mkurugenzi Mtendaji wa Benki ya CRDB, Abdulmajid Msekela, alieleza fahari ya benki hiyo kushiriki kila mwaka katika bonanza hilo, akibainisha kuwa CRDB imekuwa mshirika wa maendeleo si tu kwenye michezo, bali pia katika utekelezaji wa miradi ya kijamii ndani ya majimbo ya wabunge.

Grand Bunge Bonanza limeendelea kuwa siyo tu tukio la michezo, bali jukwaa la kuonesha mshikamano wa kitaifa, kusherehekea afya na kuleta maendeleo ya kijamii kwa kupitia ushirikiano wa sekta mbalimbali. Wadau wengi wamelitaja bonanza hilo kama urithi mzuri wa Bunge la 12, na mfano wa kuigwa kwa mabunge yajayo.