March 7, 2026

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

MNEC Mwaselela awataka wanasiasa kutoharibu amani kwa kutumia ndimi zao

Na Esther Macha,TimesmajiraOnline,Mbeya

MJUMBE wa Halmashauri Kuu ya Chama Cha Mapinduzi (CCM)Taifa(MNEC)Ndele Mwaselela amewataka wanasiasa kutumia ndimi zao vyema katika majukwaa yao na kuepuka kutumia ndimi hizo kuwa moto kwa Taifa  na kuiharibu amani ya Nchi.

Mwaselela amesema hayo Juni,22,2025  wakati aliposhiriki Ibada ya kuliombea Taifa la Tanzania na Viongozi  wote wakiongozwa na Rais Dkt.Saimia Suluhu Hassan ibada iliyofanyika katika ukumbi wa mkapa Jijini Mbeya.

“Tunapoelekea Kwenye uchaguzi mkuu Ndugu zangu wanasiasa tuepuke kutumia ndimi zetu vibaya katika majukwaa yetu kwa maana yanaweza kuharibu amani ya nchi yetu “amesema Ndele Mwaselela.

Akiendelea kuongea katika maombezi ya kuliombea Taifa MNEC Mwaselela amewaomba watumishi na waumini wote kuombea amani nchi  pamoja na Rais ili mwenyezi Mungu amwongoze kwa kadri mapenzi yake na hekima katika Taifa letu.

Aidha Mwaselela amesema kuwa wanaenda kwenye Uchaguzi kama CCM kinaenda kushindana hivyo ni lazima kumuomba Mungu ili kuweza kupata viongozi wenye hofu ya Mungu kama ilivyo kwa Rais wetu.

“Tuna kila sababu za kuhakikisha tunafanya maombi ili kuweza kupata viongozi walio bora na siyo bora viongozi,tuchague viongozi wenye maono ambao watakisaidia chama cha Mapinduzi  katika kutatua changamoto za wananchi “amesema MNEC Mwaselela.

Hata hivyo  Mwaselela amechangia Kiasi  cha shilingi Mil.2 kwa ajili ya huduma ya Uimbaji na Uinjilishaji Katika Mkoa Wa Mbeya.