March 7, 2026

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

NHIF yahimiza matumizi ya Teknolojia na elimu kwa jamii magonjwa yasiyoambukiza

Na Joyce Kasiki, TimesMajira Online – Dodoma

KATIKA kuadhimisha Wiki ya Utumishi wa Umma mwaka huu, Mfuko wa Taifa wa Bima ya Afya (NHIF) umetumia nafasi hiyo kuhamasisha matumizi ya mifumo ya kidigitali na elimu kuhusu magonjwa yasiyoambukiza, ambayo yamekuwa mzigo mkubwa kwa mfumo wa afya nchini. Hayo yameelezwa na Mkuu wa Kitengo cha Uhusiano wa NHIF, Bw. James Mlowe, wakati wa mahojiano maalum yaliyofanyika katika viwanja vya maadhimisho hayo jijini Dodoma.

Akizungumzana waandishi wa habari Jini 19,2025 kwenye bada la NHIF   Mlowe alisema kuwa “eneo la magonjwa yasiyo ya kuambukiza limekuwa changamoto kubwa kutokana na mfumo wa maisha ya sasa. Tunaona ongezeko la maradhi kama kisukari, shinikizo la damu na magonjwa ya moyo. Kwa mwaka mmoja, NHIF inalipa wastani wa shilingi bilioni 700 kwa ajili ya matibabu ya wanachama wake, ambapo zaidi ya asilimia 60 ya fedha hizo hutumika kutibu magonjwa haya yasiyo ya kuambukiza.”

Alifafanua kuwa elimu kwa jamii kuhusu namna ya kujikinga na magonjwa hayo ni jambo la msingi na ndiyo maana NHIF inatilia mkazo mkubwa suala hilo katika maadhimisho haya. Aliongeza kuwa, ikiwa jamii itapatiwa elimu sahihi, basi itawezekana kupunguza gharama kubwa zinazotumika katika matibabu na fedha hizo kuelekezwa katika upanuzi wa huduma za afya nchini.

Katika kuelekea matumizi ya teknolojia ya kisasa, Bw. Mlowe alibainisha kuwa NHIF imepiga hatua kubwa kwa kuanzisha mfumo wa “NHIF Jihudumie” ambao unamuwezesha mwanachama kujisajili, kuangalia michango, kuongeza wategemezi, na hata kupata kadi ya bima ya afya kupitia simu ya mkononi bila ya kulazimika kufika ofisi za NHIF.

Mfumo huu umeleta mapinduzi makubwa katika utoaji wa huduma kwa wanachama wetu. Mwanachama anaweza kuonesha kadi yake ya kidigitali kwenye simu katika zaidi ya vituo 10,000 vya afya vilivyosajiliwa na NHIF nchini kote na kupata huduma bila usumbufu wowote, alisema Mlowe.

Kauli mbiu ya mwaka huu ya Wiki ya Utumishi wa Umma inayozingatia matumizi ya teknolojia katika kuboresha utendaji kazi wa taasisi za umma, imetajwa na NHIF kuwa dira inayowaongoza katika mabadiliko haya ya kidigitali kwa lengo la kuwafikia watanzania wote kwa haraka na ufanisi.

Kuhusu upanuzi wa huduma, Mlowe alizungumzia pia utekelezaji wa Sheria ya Bima ya Afya kwa Wote ya mwaka 2023, akisema kuwa NHIF sasa inawafikia wananchi wote, siyo watumishi wa umma pekee kama ilivyokuwa awali. “Tuna vifurushi kama Toto Afya Kadi kwa ajili ya watoto hadi miaka 21 na kifurushi cha Tarangire kwa wajasiriamali. Vifurushi hivi vinapatikana moja kwa moja kupitia mfumo wa Jihudumie,” alieleza.

Kwa ujumla, NHIF inachukua nafasi kubwa katika kuhakikisha afya bora kwa wote, huku ikikabiliana na changamoto ya magonjwa yasiyoambukiza kwa njia ya elimu, teknolojia na upatikanaji rahisi wa huduma za bima ya afya kwa kila Mtanzania.

> “Tunaposhiriki maadhimisho haya, lengo letu kuu ni kuelimisha, kuwahudumia na kuhakikisha kila mwananchi anapata haki yake ya msingi ya huduma bora za afya,” alihitimisha Mlowe.