March 7, 2026

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Naibu Waziri Deus Sangu Aipongeza TASAF kwa Kazi Kubwa ya Kuwezesha Kaya Masikini Kiuchumi

Na Joyce Kasiki,Timesmajira online,Dodoma

NAIBU Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais – Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Deus Sangu ametembelea banda la Mfuko wa Maendeleo ya Jamii (TASAF) katika maadhimisho ya Wiki ya Utumishi wa Umma na kuipongeza taasisi hiyo kwa kazi kubwa wanayoifanya ya kuwawezesha kaya masikini kuimarika kiuchumi kupitia Mpango wa Kunusuru Kaya Masikini.

Katika ziara hiyo, Sangu aliwapongeza wataalamu wa TASAF kwa maandalizi mazuri ya kushiriki katika maadhimisho hayo, huku akisema kuwa taasisi hiyo imeitendea haki wiki hiyo kwa kuonyesha kwa vitendo matokeo ya uwekezaji wa Serikali katika kaya masikini.

“Wanufaika hawa wa TASAF ni kielelezo tosha cha mafanikio wamewezeshwa, wamejituma, na sasa ni wajasiriamali waliokomaa,wameonyesha wazi kuwa uwekezaji wa Serikali kupitia TASAF haujaenda bure,” amesema Sangu.

Maonesho hayo yalishirikisha baadhi ya walengwa wa Mpango wa TASAF, wengine wakiwa tayari wamehitimu kutoka kwenye Mpango huo huku wengine wakiendelea kunufaika. Miongoni mwa walengwa waliojitokeza ni Ummy, ambaye baada ya kupata mafunzo ya ujasiriamali, elimu ya afya, na utunzaji wa fedha kupitia TASAF, sasa ni mzalishaji wa bidhaa mbalimbali zikiwemo unga wa lishe, sabuni ya maji, peanut butter, dawa za kusafishia vyoo, sabuni za kuondoa madoa, na nguo za batiki.

Mlengwa mwingine ni Halina Mtulia, kutoka Wilaya ya Mkuranga, Mkoa wa Pwani, ambaye sasa ni mjasiriamali anayetengeneza fagio za chelewa, mikeka, vikapu, vipepeo, na makawa, bidhaa zinazopendwa na watu wengi kutokana na ubunifu wake.

Sangu amewataka wanufaika hao kutokuishia kwenye mafanikio ya awali bali waunganishwe na fursa nyingine rasmi za kiuchumi kama mikopo ya asilimia 10 ya Halmashauri, pamoja na mifuko mingine ya Serikali chini ya Ofisi ya Waziri Mkuu inayolenga kuwawezesha wananchi kiuchumi.

Amesisitiza kuwa mfano wa TASAF unaweza kuigwa kama inavyofanyika kwa wanufaika wa mikopo ya elimu kupitia Bodi ya Mikopo ya Elimu ya Juu.

“Niwapongeze kwa dhati nyote mlioshiriki maonesho haya. Hii ni safari ya mafanikio. Lakini safari hii bado ina hatua. Serikali ya Dkt. Samia Suluhu Hassan itaendelea kuwasapoti hadi mfikie hatua kubwa zaidi kiuchumi,” aliongeza.

Kwa upande wake Afisa Habari wa TASAF ,  Merkizedeck Nduye kutoka TASAF, amesema taasisi hiyo imeendelea kuwaelimisha walengwa wake kuhusu njia bora za kujikwamua kiuchumi.

 Amebainisha kuwa mbali na kushiriki kwenye maonesho hayo, wapo walengwa wengi zaidi walioweza kuhitimu kutoka kwenye Mpango na sasa wana uwezo wa kujitegemea katika mahitaji ya familia, elimu, na afya.

“Tumeshapokea maelekezo ya kuwaunganisha wanufaika na fursa mbalimbali. Kwa kweli, hata kabla ya agizo hilo rasmi, tayari tumekuwa tukifanya hivyo. Tumewasiliana na Halmashauri na baadhi ya wanufaika wetu tayari wamepata mikopo kupitia asilimia 10 za Halmashauri. Ushirikiano unaendelea kuimarika,” alisema Nduye.

Aidha, amemshukuru Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, kwa kuendelea kuiamini na kuisapoti TASAF pamoja na walengwa wake, huku akiahidi kuwa taasisi hiyo itaendelea kushirikiana na taasisi zote zenye nia ya kweli ya kuondoa umasikini nchini.

“Naibu Waziri ameona mwenyewe. Matokeo ni makubwa, yanaonekana. Na sisi kama TASAF tupo tayari kuendelea kushirikiana na Serikali kuhakikisha tunawafikia wananchi wengi zaidi na kuwasaidia kupambana na umasikini,” amesema