March 7, 2026

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Prof. Patrick Ndakidemi: “Bajeti ya Serikali 2025/2026 ni ya matumaini

Na Joyce Kasiki, Timesmajira online,odoma

MBUNGE  wa Jimbo la Moshi Vijijini, Prof. Patrick Ndakidemi, amepongeza na kuunga mkono Bajeti Kuu ya Serikali kwa mwaka wa fedha 2025/2026 akisema kuwa ni bajeti yenye mwelekeo chanya, inayolenga kutatua changamoto za wananchi na kusukuma mbele maendeleo ya taifa kwa ujumla.

Akichangia mjadala wa bajeti hiyo bungeni jijini Dodoma Juni 16 mwaka huu , Prof. Ndakidemi amesema kuwa bajeti hiyo imeonesha dhamira ya dhati ya Serikali kuendeleza miradi ya kimkakati pamoja na kuibua na kutekeleza miradi mipya kwa ajili ya kukuza uchumi na kuboresha maisha ya wananchi.

“Serikali imeongeza bajeti kutoka shilingi trilioni 50.26 hadi trilioni 56.49, ikiwa ni ongezeko la trilioni 6.2, sawa na asilimia 12.3. Hili ni jambo la kupongeza kwa kuwa linaonyesha nia ya kweli ya Serikali kuongeza uwekezaji katika maendeleo ya watu,” amesema Prof. Ndakidemi.

Afueni kwa Wakulima na Wananchi

Akigusia baadhi ya maeneo yaliyomfurahisha kwenye bajeti hiyo, Prof. Ndakidemi amepongeza uamuzi wa Serikali kuondoa tozo na kodi kwenye baadhi ya bidhaa muhimu ikiwemo viuatilifu na mbolea zinazotengenezwa hapa nchini. 

Amesema,hatua hiyo inalenga kumpunguzia mkulima mzigo wa gharama za uzalishaji na hivyo kuongeza tija katika kilimo.

“Hii ni hatua ya busara. Tunapomsaidia mkulima kwa kumwekea mazingira wezeshi ya uzalishaji, tunachochea maendeleo ya sekta ya kilimo ambayo ni uti wa mgongo wa uchumi wetu,” alisisitiza.

Mfuko Maalum wa Afya kwa Watu Wenye Uhitaji

Katika hatua nyingine, Prof. Ndakidemi amepongeza uanzishwaji wa Mfuko Maalum wa Afya, ambao utahudumia makundi maalum ya wananchi wakiwemo watu wanaoishi na virusi vya UKIMWI, akinamama wajawazito, wazee na watoto.

Mfuko huo utapata fedha kutoka kwenye vyanzo mbalimbali vya ndani kama vile kodi ya vinywaji vikali vinavyoagizwa kutoka nje, tozo ya mafuta, barabara, na michezo ya kubahatisha.

“Mfuko huu ukisimamiwa vizuri utasaidia sana katika kupunguza mzigo wa gharama za huduma za afya kwa wananchi wasio na uwezo. Pia nashauri makundi maalum kama wale wasiokuwa katika ajira rasmi ya Serikali waangaliwe upya ili waweze kupata pensheni kama ilivyo kwa upande wa Zanzibar,” alishauri Prof. Ndakidemi.

Kuongezeka kwa Pensheni ya Wazee

Prof. Ndakidemi pia ameipongeza Serikali kwa hatua ya kuongeza pensheni ya wazee kutoka kiwango cha chini cha shilingi 100,000 hadi kufikia shilingi 250,000. Ameeleza kuwa hatua hiyo ni ya kipekee na inaonesha jinsi Serikali inavyowathamini wazee waliolitumikia taifa kwa muda mrefu.

Mafanikio Jimboni Moshi Vijijini

Kwa upande wa utekelezaji wa Ilani ya Chama cha Mapinduzi katika Jimbo la Moshi Vijijini, Prof. Ndakidemi amesema kuwa mafanikio ni makubwa, akitaja maendeleo ya barabara, huduma za maji safi, miundombinu ya elimu na afya kuwa miongoni mwa maeneo yaliyopata msukumo mkubwa wa maendeleo.

“Naipongeza Serikali kwa kutimiza ahadi zake kwa wananchi. Miradi mingi iliyopangwa katika Ilani ya Uchaguzi imetekelezwa kwa kiwango kikubwa, na hii ni faraja kwa wananchi wa Moshi Vijijini,” alisema.

Prof. Ndakidemi amehitimisha kwa kuitaka Serikali kuhakikisha utekelezaji wa bajeti hiyo unazingatia ufanisi, uwazi, na usimamizi thabiti wa rasilimali, ili kuhakikisha kuwa matumaini makubwa yaliyowekwa kwa bajeti hii yanazaa matunda kwa Watanzania wote.