June 18, 2025

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

CTI yampongeza Samia kwa bajeti itakayokuza uchumi

Na Mwandishi Wetu,Timesmajiraonline, Dar

SHIRIKISHO la Wenye Viwanda Tanzania (CTI), limempongeza Rais Samia Suluhu Hassan kwa bajeti nzuri na shirikishi likisema kwamba inajaribu kuweka uwiano kati ya kukusanya mapato zaidi kutoka vyanzo vya ndani na kuweka mikakati inayolenga kuchochea ukuaji wa uchumi.

Makamu Mwenyekiti wa CTI, Hussein Sufiani aliwaambia waandishi wa habari jana jijini Dar es Salaam kuwa wametiwa moyo sana na hotuba ya bajeti inayoonyesha ari ya serikali katika kuleta mageuzi jumuishi ya kiuchumi kupitia uhamasishaji wa rasilimali za ndani na uwekezaji wa kimkakati wa kuzalisha ajira na kuboresha maisha.

“Ahadi hii inaonekana wazi katika bajeti kupitia mpango wa Serikali wa kufanyia kazi mwongozo wa pili wa maboresho ya udhibiti ili kuboresha mazingira ya biashara kwa lengo la kuwezesha uwekezaji wa ndani na nje,” alisema Sufian.

Alisema jambo muhimu katika bajeti ya mwaka huu ni serikali kuanzisha marekebisho mbalimbali ya muundo wa kodi, ada, tozo na marekebisho ya sheria na kanuni kwa lengo la kuimarisha mazingira ya biashara.

Alisema mageuzi yanayopendekezwa yanalenga kukuza mageuzi endelevu ya kiuchumi kwa kulinda viwanda vya ndani; kuongeza uwezo wa uzalishaji wa ndani na kuboresha ushindani wa bidhaa zinazozalishwa katika soko la ndani, kikanda na kimataifa.

Aliongeza kuwa mageuzi hayo pia yanalenga kukuza uongezaji thamani wa ndani, kupunguza utegemezi wa bidhaa kutoka nje, na kuhimiza ukuaji wa viwanda, kwa lengo pana la kutengeneza ajira na kuleta utulivu wa bei huku kukiwa na shinikizo la mfumuko wa bei.

Alisema kuondolewa kwa ada ya leseni ya Tsh. 300,000 kwa wazalishaji na waagizaji wa bidhaa zinazotozwa ushuru inakusudiwa kupunguza gharama za uzalishaji na uagizaji wa bidhaa zinazotozwa ushuru, kulingana na lengo la serikali la kupunguza gharama za kufanya biashara nchini.

Sufian alisema katika mwaka wa Fedha 2023/2024 serikali ilianzisha kalenda ya miaka mitatu ya ushuru wa bidhaa, ikimaanisha kuwa hakutakuwa na ongezeko la ushuru katika kipindi cha miaka mitatu.

Alisema CTI inaishukuru serikali kwa kuweka zuio la ongezeko la ushuru kwa miaka mitatu kwani inaleta hali ya kutabirika.

Hata hivyo, alisema hotuba ya bajeti imependekeza marekebisho ya Sheria ya Ushuru kuongeza kiwango cha ushuru wa bidhaa kwa shilingi 20 kwa lita kwa bia chini ya kifungu cha 22.03; shilingi 30 kwa lita kwa mvinyo na vinywaji vingine vilivyochachushwa.

“Hatua hii imekuja kwa mshangao na hatimaye itakuwa na athari kubwa kwa viwanda kuongezeka kwa gharama za uzalishaji na mipango ya uzalishaji wa makampuni,” alisema Sufian.

Alisema katika bajeti hiyo kuna kuanzishwa kwa ushuru wa asilimia tano kwenye soseji zinazotengenezwa nchini na kuongeza kuwa sekta hiyo ndogo inahitaji kupata msaada wa serikali ili kuwezesha ukuaji wake.

Sufiani alisema kuanzishwa kwa ushuru huo kutakuwa na athari mbaya katika ukuaji wa sekta hii ndogo.

Alisema CTI inaamini kuwa vipaumbele vilivyochaguliwa kwa mwaka wa fedha 2025/2026 vitachangia ipasavyo katika maendeleo endelevu ya sekta ya viwanda nchini.

“CTI inaamini kuwa bajeti ya 2025/2026 ikitekelezwa ipasavyo, Serikali itaimarisha ukusanyaji wa mapato ya ndani, kuendeleza ukuaji wa uchumi, kuimarisha miundombinu na huduma za umma,” alisema

Alisema hali hiyo itawezesha kufikia maendeleo mapana ya kiuchumi na aliahidi kuwa CTI itashirikiana bega kwa bega na serikali ya awamu ya sita ili kufikia malengo yaliyowekwa ya kijamii na kiuchumi.