Na Mwanidishi Wetu, Timesmajira
RAIS wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. Samia Suluhu Hassan ametoa ruzuku ya Shilingi Bil. 216 kwenye kampeni ya kuchanja mifugo na utambuzi kwa kipindi cha miaka 5 kuanzia mwaka huu.
Akizungumza katika hafla ya Uzinduzi wa kampeni ya kitaifa ya chanjo hizo na Utambuzi wa Mifugo iliyofanyika kwenye Viwanja vya Nyakabindi mkoani simiyu, Dkt. Samia amewataka Wakuu wa Mikoa yote nchini kusimamia matumizi ya vifaa hivyo na kuhakikisha vinatumika kwa maslahi ya wafugaji kama ilivyokusudiwa.
Aidha Dkt. Samia amebainisha kuwa hivi sasa Serikali imeanza kuona matunda ya mabadiliko ya ufugaji wa kisasa yaliyofanyika ambapo ameongeza kuwa Serikali itaendelea kuboresha sekta hiyo ili tija iendelee kuonekana.
“Serikali imedhamiria kutokomeza magonjwa ya Mifugo na ndio maana leo tunazindua mpango huu wa chanjo 2025/2029 na hapa kwa dhati kabisa nataka niwapongeze kabisa wafugaji wote Tanzania kwa sababu mmekubali kuchangia nusu na sisi Serikali tutoe nusu kwenye chanjo ya Ng’ombe, Mbuzi na Kondoo” Ameongeza Dkt. Samia
Aidha Dkt. Samia amebainisha kuwa baada ya kutoa ruzuku kwenye sekta ya kilimo, Serikali imeanza kutoa ruzuku kwenye sekta ya Mifugo kwa upande wa chanjo za Mifugo.
Dkt. Samia amesema kuwa Serikali imeweka mazingira wezeshi kwa sekta ya umma na sekta binafsi ambazo zimetengeneza chanjo zitakazotumika kwenye kampeni hiyo na amefarijika na mipango yao ya kuhakikisha Tanzania inajitegemea kwa upande wa chanjo za mifugo nchini.
“Tulipokuwa tukiagiza wakati mwingine tunakuwa na mashaka kuhusu usalama wa chanjo tunazotumia lakini sasa kwa kuwa zimetengenezwa hapa hapa na wazawa inatuongezea imani ya chanjo zilizopo hivyo niipongeze Wizara kwa uamuzi huo wa kutumia wazalishaji wa ndani kwenye upande huu.
Akizungumzia kuhusu hereni za kielektroniki Mhe. Dkt. Samia amesema kuwa kwa muda mrefu Serikali imekuaa ikikisia kuhusu kanzidata ya Mifugo iliyopo nchini hivyo hereni hizo zitakuwa ni nyenzo ya upatikanaji wa kanzidata hizo.
Akizungumza kabla ya kumkaribisha Mhe. Rais, Waziri wa Mifugo na Uvuvi Mhe. Dkt. Ashatu Kijaji mbali na kumshukuru Mhe. Dkt. samia kwa kutoa ruzuku hiyo amesema kuwa tayari Wizara yake imeshanunua vifaa vya kutekelezea zoezi hilo kwa awamu ya kwanza ambavyo ni pamoja na vifaa vya kutolea chanjo, pikipiki 700 na vishkwambi 4500 vitakavyotolewa kwa Maafisa mifugo kwenye Halmashauri zote nchini.
Dkt. Kijaji ameongeza kuwa katika kampeni hiyo wanaratajia kuchanja magonjwa 5 ambayo ni Homa ya mapafu kwa upande wa Ng’ombe, Sotoka kwa upande wa Mbuzi na Kondoo, Kideri/mdondo, Ndui na mafua ya kuku kwa upande wa kuku wa kienyeji.
“Aidha zoezi hili linatarajiwa kuzalisha ajira za muda mfupi 3540 ambazo zitahusisha wataalam wa afya ya Mifugo waliopo nje ya mfumo rasmi wa ajira.
Chanjo hizo zilizozalishwa na viwanda vilivyopo hapa nchini zitatolewa kwa kufuata mwongozo wa uliotolewa na Wizara hiyo ambapo ng’ombe atachanjwa kwa shilingi 500 badala ya 1000 iliyokuwa awali, mbuzi na kondoo watachanjwa kwa shilingi 300 badala ya 600 ya awali huku chanjo ya kukabiliana na magonjwa ya kuku ikitolewa bure.
Mwiahoooo
More Stories
REA yaendelea kusambaza Nishati Bora kwa wananchi,yamshukuru Rais Dkt.Samia
Vivo Energy Tanzania, yazindua Kampeni ya “Uliza Oili ya Shell”
Kampeni ya kisheria ya Mama Samia kuondoa migogoro na ukatili