Na Yusuph Mussa,Timesmajiraonline,Tanga
KIONGOZI wa Mbio za Mwenge wa Uhuru kitaifa Ismail Ali Ussi amesema ufungaji wa dira za maji za malipo ya kabla kwa wananchi wote kutaondoa malalamiko ya kutopata maji kwa wakati, ama kwa wale wanaodai wametumia maji kidogo, lakini ankara ya maji inakuja kubwa.
Ameyasema hayo Juni 16, 2025 alipofika kwenye mradi wa ufungaji wa dira za maji za malipo ya kabla Awamu ya Kwanza unaofanywa na Mamlaka ya Maji Safi na Usafi wa Mazingira Tanga (Tanga- UWASA), ambapo zoezi hilo lilifanyika Jengo la Huduma kwa Wateja wa Tanga- UWASA, Mtaa wa Mwakidila katika Jiji la Tanga.

“Wananchi wa Mwakidila leo hii ni siku ya faraja kwetu sababu tunakwenda kuondosha kabisa changamoto ya muda mrefu iliyokuwa inawapata wananchi. Wananchi wetu walikuwa wanapata maji, lakini walikuwa hawayapati kwa muda unaostahili. Na wengine kupelekea changamoto ya kwamba, mimi nyumbani kwangu nimechota kidogo, wenzangu wamechota mengi, jambo ambalo lilikuwa linatupa utata hata sisi viongozi na wenzetu wa Tanga- UWASA.
“Na kama sisi wengi tumejionea kwenye documentary pale, Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan aliwapa maelekezo wenzetu hawa (Tanga- UWASA), wahakikishe wanakuja na mfumo mwingine mbadala wakuweza kila mmoja asiweze kumlaumu mwenzake wa kupata maji ambayo anastahili kwa uwezo wake, na wenzetu wa Tanga- UWASA wamekuwa wasikivu na kuweza kutimiza azma hiyo”amesema Ussi.

Ussi amesema kutokana na huduma hiyo mpya, hakuna mwananchi atakwenda kumlaumu kiongozi kwa sababu miundombinu ya maji imeshawekwa, lakini ili mwananchi aweze kupata maji kwa wingi na kwa wakati, anatakiwa kuhakikisha anapata dira hiyo ya maji.
Mbunge wa Jimbo la Tanga, Ummy Mwalimu alisema kwa Tanga- UWASA kuweka dira hizo kutaondoa malalamiko ya wananchi kuwa wanabambikiwa ankara za maji, kwani hata yeye nyumbani kwake aliwahi kuona ankara ya malipo inayokuja ni kubwa kuliko matumizi yake, hivyo anamshukuru Rais Dkt. Samia kwa kuwawezesha mamlaka za maji kuja na mpango huo ambao utaleta nafuu kwa wananchi.

Akisoma taarifa hiyo, Mkurugenzi wa Huduma kwa Wateja wa Tanga- UWASA Alawi Ahmed,amesema kufuatia maagizo ya Rais Dkt. Samia kuhusu ufungaji wa dira za maji za malipo ya kabla kwa wananchi wote kwa lengo la kuboresha huduma za maji, Tanga UWASA imeanza rasmi utekelezaji wa mradi huo muhimu kwa wateja wake katika maeneo ya Tanga Jiji pamoja na Miji ya Muheza na Pangani.
“Mradi huu ulioanza kutekelezwa Julai, 2024 unagharimu sh. 1,872,091,735 na unatekelezwa kwa fedha za Serikali Kuu kupitia Wizara ya Maji chini ya Program ya IFF-OBA (Investment Financing Facility – Output Based Aid) kupitia Mfuko wa Maji wa Taifa (NWF). Aidha, utekelezaji wa mradi hadi sasa, umefikia asilimia 55.05 kwa kufunga dira 2,202 kati ya 4,000.

“Mradi wa ufungaji wa dira za maji za malipo ya kabla una faida kadhaa muhimu; Mradi huu utaongeza ufanisi wa ukusanyaji wa mapato kwa kuhakikisha malipo ya maji yanafanyika kwa wakati na kupunguza madeni ya wateja, kugundua kwa haraka uvujaji wa maji ambao husababisha ankara kubwa, kuimarisha matumizi sahihi ya maji kwa kuwa wateja watakuwa waangalifu kutokana na mfumo wa kulipia maji kabla ya kutumia hivyo kupunguza malalamiko kuhusu ankara za maji na kuboresha zaidi utoaji wa huduma za maji”amesema Ahmed.
Ahmed amesema Tanga UWASA inatoa shukrani za dhati kwa Rais Dkt.Samia kwa maono yake, miongozo yake na maelekezo ya kuimarisha huduma za maji kupitia ufungaji wa dira za maji za malipo ya kabla. Vilevile, tunatoa pongezi kwa Wizara ya Maji kwa utekelezaji na usimamizi thabiti wa agizo hili.


More Stories
REA yaendelea kusambaza Nishati Bora kwa wananchi,yamshukuru Rais Dkt.Samia
Vivo Energy Tanzania, yazindua Kampeni ya “Uliza Oili ya Shell”
Kampeni ya kisheria ya Mama Samia kuondoa migogoro na ukatili