Na Yusuph Mussa,Timesmajiraonline,Muheza
KIONGOZI wa Mbio za Mwenge wa Uhuru kitaifa Ismail Ali Ussi amesema Rais Dkt.Samia Suluhu Hassan kupeleka maji hadi vijijini kumesaidia wanawake kuondokana na adha mbalimbali ikiwemo kubakwa na kupoteza maisha kutokana na kutafuta maji usiku wa manane.
Ameyasema hayo Juni 13, 2025 wakati alipofika Kijiji cha Mkinga, Kata ya Tingeni, Wilaya ya Muheza mkoani Tanga kuweka Jiwe la Msingi Mradi wa Uchimbaji Visima vitano, na kuongeza kuwa kazi ya kupeleka maji vijijini kwa Mkoa wa Tanga imefanyika kwa kiwango kikubwa, na cha kuigwa kwa mikoa mingine.

“Tulizoea miundombinu ya maji ikiwekwa makao makuu ya wilaya au halmashauri, lakini wakati ule, Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan aliahidi kupeleka maji hadi maeneo ya vijijini na kata zao zote, na hili Rais amefanikiwa kwa asilimia 100. Nayasema haya ninyi wenyewe mkiwa mashuhuda, Mkuu wa Wilaya (Zainab Abdallah) amesema hapa, lakini pia Mbunge wetu (Hamis Mwinjuma. Jimbo la Muheza) amesema, na taarifa iliyowasilishwa na RUWASA, nayo imesema kuwa ndugu zetu wa Mkinga mlikuwa na changamoto ya maji safi na salama.
“Mbunge wetu ametuambia, ukiangalia maeneo mengi idadi ya wananchi ilikuwa ni ndogo kuliko madumu ya maji. Kwanza tulikuwa tunayapata maeneo ya mbali, pili ilikuwa inatupelekea changamoto, kama mlikuwa na mimi wakati naangalia documentary, wananchi wenyewe walikuwa wanasema, wengine tumeshapoteza hata wazazi wetu kwenye hili suala la kutafuta maji, lakini Rais Dkt. Samia akasikia kilio hicho akaona ipo haja ya kuhakikisha anaikamilisha kampeni hii inakamilika” amesema Ussi.

Akisoma taarifa ya mradi huo, Meneja wa RUWASA Wilaya ya Muheza Mhandisi Cleophace Maharangata amesema
wanatekeleza mradi wa uchimbaji na uendelezaji wa visima vitano ambao ni sehemu ya Utekelezaji wa Mpango wa Uchimbaji na Uendelezaji wa Visima 900 nchini. Utafiti, uchimbaji na uendelezaji wa visima hivyo unafanyika katika vijiji vya Kibanda, Mkinga, Tingeni, Mindu na Mbambara.
“Mradi huu unatekelezwa na Mkandarasi JNB Construction Company Ltd ambaye amechimba visima pamoja na Mkandarasi Frangem International Ltd ambaye anatekeleza ujenzi wa miundombinu ya kuchotea maji kwa jumla ya sh. 291,085,632 kupitia mpango wa malipo kwa matokeo (PforR).

“Utekelezaji wa mradi huu ulianza Novemba Mosi, 2024 na unatarajiwa kukamilika Julai 13, 2025. Kazi zilizotekelezwa ni pamoja na:
Utafiti wa maji chini ya ardhi imekamilika kwa asilimia 100,
uchimbaji wa visima vitano asilimia 100, ujenzi wa miundombinu ya kuchotea maji- asilimia 60, ununuzi na ufungaji wa tenki la maji lita 10,000 asilimia 60,
uunganishaji wa nishati ya umeme asilimia 60, ununuzi na ufungaji wa pampu asilimia 60 na ujenzi wa fensi asilimia 50″ amesema Mhandisi Maharangata.
Mhandisi Maharangata amesema mradi huo umefikia asilimia 75 ya utekelezaji na kiasi cha sh. 137,686,899 kimeshatumika, na utakapokamilika utanufaisha wananchi 3,950 waliopo katika maeneo ya mradi.
“Tunamshukuru sana Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kutupatia fedha za utekelezaji wa mradi huu” amesema Mhandisi Maharangata.



More Stories
Aweso:Rais Samia ameweza kumtua mwanamke ndoo kichwani
Jukwaa la wanawake Ilala laadhimia kumuunga mkono Rais Samia
TPTC kuendelea kuendesha kozi ya ulinzi wa amani kwa Watanzania