Na Yusuph Mussa,Timesmajiraonline,Korogwe
KIONGOZI wa Mbio za Mwenge wa Uhuru Ismail Ali Ussi amesema dhamira ya dhati ya Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kumtua ndoo kichwani mwanamke wa Kitanzania imetimia, kwani amekuwa akiona miradi ya maji kwenye kona zote za nchi ikiwemo halmashauri za Mkoa wa Tanga.
Akizungumza Juni 12, 2025 alipofika kuweka Jiwe la Ufunguzi Mradi wa Maji Magila- Gereza uliopo Kijiji cha Nkalekwa, Kata ya Magila- Gereza, Halmashauri ya Wilaya ya Korogwe, ameongeza kuwa maji hayo yamesaidia kuwaondolea shida ya maji wananchi kwenye miji na vijiji vyao.

“Tumekuja kujionea miradi mikubwa ambayo inaendelea kusimamiwa na kutekelezwa na Serikali hii ya Awamu ya Sita chini ya Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan. Kwa kweli hii miundombinu ya maji safi na salama katika Taifa letu kwa kweli tumekwenda kuondosha changamoto kabisa katika maeneo yote. Nathubutu kusema maeneo yote kwa sababu leo hii Serikali ya Dkt. Samia kupitia Wizara ya Maji, kwa kweli kupitia taasisi yetu ya RUWASA ambayo ina jukumu la kutatua changamoto za wananchi juu ya miundombinu ya maji safi na salama vijijini, kwa kweli imeendelea kufanya vizuri.
“Lakini pia, katika eneo hili la Nkalekwa tunaendelea kujionea maana halisi ya Mwenge wa Uhuru kuwashwa kwake na kukimbizwa kwake hapa nchini. Tumeambiwa katika taarifa ambayo imesomwa hapa na afisa wetu kutoka RUWASA, kwamba Mwenge wa Uhuru katika eneo hili mwaka wa jana uliweka Jiwe la Msingi kwenye huu mradi wa maji, lakini leo hii muda si mrefu utakwenda kuzindua mradi huu wa maji safi na salama kwa wananchi wetu wa Nkalekwa.

Ussi amesema Rais Dkt. Samia wakati anahutubia Bunge kwa mara ya kwanza Aprili 22, 2021, aliahidi kutatua tatizo la maji kwa wananchi, na katika kutimiza azma hiyo, amefanya jitihada mbalimbali za kujenga miundombinu ya maji kuanzia kwenye vyanzo, na kule kusikokuwa na vyanzo vya maji alipeleka magari yenye mitambo ya kujichamba visima virefu kupitia mradi wa visima 900 nchini.
“Wenyewe mmejionea kupitia Serikali ya Awamu ya Sita ya Dkt. Samia, kwamba aliwaahidi wananchi kwamba nitahakikisha naboresha miundombinu ya maji safi na salama, na ndiyo maana leo hii vijiji vyote na kata zote zina miundombinu ya maji safi na salama, na hatukutarajia leo hii eneo hili miundombinu ya maji ya bomba itafika mpaka kwenye makazi yetu. Wakati napitia taarifa yenu, ilionesha mlikuwa na changamoto kubwa ya maji safi na salama, lakini leo hii maji yapo kwenye maeneo yenu, hii ni faraja kwenu kwa Serikali ya Awamu ya Sita, ombi langu muitunze na kuilinda miundombinu hii ya maji safi na salama” amesema Ussi.
Akisoma taarifa ya mradi huo, Meneja wa Wakala wa Maji Safi na Usafi wa Mazingira (RUWASA) Wilaya ya Korogwe Mhandisi Muharami Mohamed amesema Mradi wa Maji Magila- Gereza ulianza kutekelezwa mnamo Mei 31, 2022 kwa kutumia Mkandarasi M/s YAJUKI INVESTIMENT CO. LTD wa Dar es salaam.

Lengo la mradi huo ni kutekeleza azma ya Serikali ya kuondoa kero ya maji kwa wananchi wapatao 6,394 wa vijiji vya Magila- Gereza, Nkalekwa na Mgobe. Mradi huo umekamilika kwa asilimia 100 mnamo Septemba 30, 2024 na wananchi wanapata huduma ya maji. Gharama ya mradi huo hadi kukamilika kwake ni sh. 775,743,809 kupitia Mfuko wa Taifa wa Maji (NWF). Mkandarasi ameshalipwa sh. 521,864,123.
“Mradi huu uliwekewa Jiwe la Msingi mwaka 2024 na Kiongozi wa Mbio za Mwenge wa Uhuru, 2024 Godfrey Eliakim Mnzava kwa kazi zilizokuwa zimetekelezwa ambazo ni ujenzi wa chanzo cha maji upo asilimia 95, tanki la ujazo wa lita 300,000 kwa asilimia 95, BPT 5 kwa asilimia 95, mtaro na kufunga mabomba mita 26,314 kwa asilimia 80, Vilula (DPs) 28 kwa asilimia 90, alama za njia ya bomba 264 kwa asilimia 20 na valvu chemba 34 kwa asilimia sifuri” amesema Mhandisi Mohamed.

“Kazi zilizokuwa zimebaki kwa mujibu wa mkataba na zimetekelezwa ni ujenzi wa chanzo cha maji, tenki la ujazo wa lita 300,000, ujenzi wa BPT 5, uchimbaji wa mtaro na kufunga mabomba mita 26,314, ujenzi wa vilula (DPs) 28, alama za njia ya bomba 264, valvu chemba 34 na ujenzi wa fensi kwenye tenki, na kazi hizi zote zimekamilika kwa asilimia 100” amesema Mhandisi Mohamed.
Mhandisi Mohamed, kwa niaba ya wananchi, wamemshukuru Rais Dkt. Samia kwa kuondoa kero ya maji kwa wananchi wa Magila- Gereza, Nkalekwa na Mgobe. Pia amewezesha wananchi zaidi ya 95 kupata ajira ya muda katika kipindi chote cha ujenzi wa mradi huo. Na ili mradi huo uwe endelevu, wananchi wameshirikishwa katika hatua zote za utekelezaji wa mradi huo. Kwa sasa kimeundwa chombo cha kijamii cha Watumia Maji (CBWSO) kama ilivyoainishwa kwenye Sheria Na.5 ya Maji na Usafi wa Mazingira ya mwaka 2019.Â

More Stories
WMA yafikia asilimia 96 utekelezaji mpango kazi wa Mwaka
Kamishna wa umeme na nishati jadidifu afanya ziara ya ukaguzi wa miradi ya umeme jijini Dar
Majaliwa:Wanufaikaji Mikopo ya Elimu ya Juu kuongezeka