Skimu ya Mkotamo kunufaisha wakulima 497 kwa kilimo cha mpunga na mbogamboga
Na Mwandishi Wetu, TimesMajira Online,

SERIKALI kupitia Tume ya Taifa ya Umwagiliaji (NIRC) imewekeza zaidi ya shilingi bilioni 3 kwa ajili ya ujenzi wa miundombinu ya umwagiliaji katika skimu ya Mkotamo, wilayani Tunduru, mkoani Ruvuma.
Uwekezaji huo mkubwa unalenga kuwanufaisha wakulima zaidi ya 497 kwa kuwapatia maji ya uhakika kwa ajili ya kilimo cha mpunga na mbogamboga katika eneo lenye jumla ya ekari 867.
Akizungumza wakati wa hafla ya utiaji saini ya ujenzi wa mradi huo, Mkuu wa Wilaya ya Tunduru, Simon Chacha, alisema mradi huo ni sehemu ya jitihada za Serikali ya Awamu ya Sita katika kuimarisha kilimo chenye tija na kuongeza pato la wananchi kupitia kilimo cha umwagiliaji.

“Kilimo ndicho uti wa mgongo wa uchumi wa wilaya yetu. Serikali imeamua kuwekeza kwenye miradi hii ili kuhakikisha wakulima wanapata maji ya uhakika kwa ajili ya kuongeza uzalishaji bila kutegemea mvua,” alisema Chacha.
Kwa mujibu wa Mkuu huyo wa wilaya, skimu hiyo itawawezesha wakulima kulima mara tatu kwa mwaka na hivyo kuongeza tija na kipato cha kaya za wakulima wadogo wilayani humo.
Kwa upande wake, Mhandisi wa Umwagiliaji Mkoa wa Ruvuma, Lucia Chaula, alisema mradi huo utaimarisha kilimo endelevu huku ukizingatia matumizi bora ya rasilimali za maji na uhifadhi wa mazingira.
“Mradi huu si tu kwamba utaongeza uzalishaji wa mazao, bali pia unaweka msingi wa maendeleo endelevu kwa kulinda vyanzo vya maji na mazingira kupitia ushirikiano wa wakulima, jamii na serikali,” alisema Mhandisi Chaula.
Alifafanua kuwa utekelezaji wa mradi huo umeanza rasmi Aprili 2025 na unatarajiwa kukamilika Aprili 2026. Kazi zitakazofanyika ni pamoja na ujenzi wa banio, mifereji mikuu na midogo ya umwagiliaji, barabara za mashambani na vivuko vya maji.
Ujenzi wa miundombinu hiyo katika skimu ya Mkotamo ni sehemu ya mkakati mpana wa serikali wa kufanikisha mapinduzi ya kilimo kupitia Mpango wa Taifa wa Umwagiliaji unaotekelezwa chini ya dhamira ya Serikali ya Awamu ya Sita, chini ya Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan.



More Stories
Waziri Mkuu kuzindua Kampeni ya msaada wa kisheria Dar
Bilioni 190 kuimarisha mafunzo ya ufundi stadi
Makongoro aielekeza Halmashauri ya Nkasi hoja za kufanyiwa kazi haraka