March 7, 2026

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Mwenezi NCCR Mageuzi atimukia ACT Wazalendo

Na Heri Shaaban,Timesmajiraonline,Dar

KATIBU Mwenezi wa Chama cha NCCR Mageuzi Taifa, Elisante Ngoma,leo amejiondoa katika chama hicho na kujiunga na chama kingine cha ACT Wazalendo .

Akizungumza na waandishi jijini hapa leo,Juni 9,2025,Ngoma amesema sababu ya kukihama chama hicho ni kupoteza dira na mweleko kwa chama hicho hivyo amelazimiaka  kujiondoa rasmi  na kujiunga ACT wazalendo ili kuongeza nguvu za kuweza kupambana pamoja na kugombea Ubunge Jimbo la Same Mangaribi.

Ngoma amesema sababu zingine za kujiunga ACT Wazalendo inatokana na Chama cha NCCR Mageuzi ni kupoteza dira ya kupambana na CCM hivyo ameachana na siasa za kuwalaghai watanzania,siasa zisizoangalia maslahi ya wananchi bali maslahi ya wachache.

Amesema awali akiwa NCCR Mageuzi amewai kuwa  Naibu Katibu Mkuu wa vijana Taifa,Katibu Mkuu wa Vijana Taifa  na Katibu Mwenezi Taifa.

“Nitakisaidia chama changu kipya cha ACT  Wazalendo nitagombea ubunge nyumbani nilipozaliwa Same Magharibi katika uchaguzi mkuu wa Rais,Wabunge na Madiwani mwaka huu 2025 nitatumia nguvu zangu zote kuondoa chama cha Mapinduzi madarakani “amesema Elisante.

Aidha ametaja sababu nyingine iliyomvutia kujiunga  ACT Wazalendo kuwa amedai ni  chama makini ambacho kina uwezo wa kuiondoa CCM madarakani kwani ni chama chenye  maslahi na jitihada za kuwalea vijana.

Amesema Wajumbe wote wa Halmashauri Kuu ya NCCR Mageuzi na wao wapo Mbioni kujiunga ACT Wazalendo kuongeza nguvu ndani ya chama hicho kiweze kushika dola.

Alitumia fursa hiyo kuwapongeza chama cha ACT Wazalendo kwa kazi nzuri  na nguvu watakayotumia mwaka huu katika uchaguzi mkuu itawawesha kuingia Ikulu.

Kwa upande wake Katibu Mkuu wa chama cha ACT Wazalendo, Ado Shaibu,amesema Ngoma ni moja ya vijana wenye nguvu na vipaji hivyo wamempokea ndani ya chama cha ACT Wazalendo  kuongeza nguvu kwa ajili ya kupeperusha Bendera ya chama hicho.

Vilevile Katibu huyo aliwataka vijana wote wanaogombea wajiunge na chama cha ACT Wazalendo kwani vijana wana nguvu na umoja huku akisema vijana wana ndoto kubwa sasa wote wapo ACT wazalendo   chama makini kinaendeshwa kizalendo.