Majaliwa Azindua Ujenzi wa Makao ya TBS, Ataka Miundombinu Kukamilika Haraka.
Na Joyce Kasiki,Timesmajira online Dodoma
WAZIRI Mkuu Kassim Majaliwa ametoa wito kwa wazalishaji wa bidhaa nchini kushirikiana kwa karibu na Shirika la Viwango Tanzania (TBS) katika hatua zote za uzalishaji wa bidhaa, ili kuhakikisha zinakidhi viwango vya ubora vinavyotakiwa na kuepuka hasara zitokanazo na kutengeneza bidhaa zisizo na sifa kwa matumizi.
Aidha ameziagiza Mamlaka zinazoshughulika na masuala ya maji,umeme na barabara kuhakikisha miundombinu ya huduma hizo inafika haraka ili kurahisisha ujenzi wa jengo hilo.
“Wakala wa Barabara za Mijini na Vijijini (TARURA),hakikisheni mnaweka lami barabara zote zinazoingia kwenye jengo hili na majengo yote ya jirani,siyo mtu anaingia hapa halafu ni vumbi tu,
“Pia watu wa TANESCO hakikisheni umeme unafika hapa haraka lakini pia na watu wa DUWASA,leteni maji haraka kazi zifanyike kwa urahisi.”amesisitiza Waziri Mkuu Majaliwa
Majaliwa ametoa maagizo hayo jijini Dodoma Juni 4,2025, wakati akiweka jiwe la msingi katika mradi wa ujenzi wa jengo jipya la makao makuu ya TBS, maarufu kama Viwango House, unaogharimu shilingi bilioni 25.3 hadi kukamilika kwake.
Kuhusu TBS amesema,Shirika la Viwango msisubiri bidhaa zitengenezwe ndipo mzifuatilie. Nendeni mapema, mshirikiane na wazalishaji kabla ya mchakato wa uzalishaji kuanza na kwa upande wa wazalishaji, hakikisheni mnawashirikisha TBS katika kila hatua ili kuhakikisha bidhaa zenu zinakidhi viwango kabla ya kuziingiza sokoni,” amesema Waziri Mkuu.
Aidha, amewataka watumiaji kuwa makini kwa kuhakikisha bidhaa wanazonunua zina nembo ya ubora ya TBS kabla ya kuzitumia, akisisitiza kuwa bidhaa isiyo na alama hiyo haifai kwa matumizi.
Kwa upande wake, Waziri wa Viwanda na Biashara Dkt. Selemani Jafo ameema ujenzi wa Viwango House umefikia hatua nzuri, huku akimhakikishia Waziri Mkuu kuwa wizara yake itahakikisha mradi huo unakamilika kwa wakati kama ilivyopangwa.
“Jengo hili likikamilika litakuwa na maabara kubwa zitakazosaidia nchi kujitegemea katika upimaji wa viwango vya bidhaa, hasa vyakula. Hatutalazimika tena kupeleka sampuli nje ya nchi kwa vipimo,” alisema Dkt. Jafo.
Naye Mkurugenzi Mkuu wa TBS, Dkt. Ashura Abdul Katunzi, alisema hadi sasa mradi wa ujenzi huo umefikia asilimia 70 na unatarajiwa kukamilika mwezi Agosti mwaka huu.
Amebainisha kuwa kazi zinazoendelea kwa sasa ni usimikaji wa madirisha na upakaji wa rangi.
Dkt. Katunzi ameeleza kuwa jengo hilo litaboresha utoaji wa huduma za TBS katika Kanda ya Kati na mikoa jirani, huku akisema shirika hilo kwa sasa linaendesha maabara 12 na ofisi za kanda saba, na linaendelea kujenga ofisi zaidi kwa kutumia fedha za ndani.
More Stories
Naibu Waziri Nderiananga awasilisha salamu za pole msiba wa mdogo wake Lukuvi
Kiongozi wa Mwenge apongeza wananchi kupelekewa huduma ya maji Handeni
TFS yawakaribisha wawekezaji katika vivutio vya utalii wa misitu