Na Mwandishi wetu,Timesmajira
Utekelezaji wa mradi wa Bomba la Mafuta Ghafi Afrika Mashariki (EACOP), unaojumuisha ujenzi wa bomba la urefu wa kilomita 1,443 kutoka Hoima nchini Uganda hadi Chongoleani, Tanga – Tanzania, umefikia asilimia 60 ya utekelezaji.
Taarifa hiyo ilitolewa tarehe 2 Juni 2025, wakati Bodi ya Wakurugenzi ya Mamlaka ya Udhibiti wa Huduma za Nishati na Maji (EWURA) ilipofanya ziara ya ukaguzi wa mradi huo katika eneo la Chongoleani, mkoani Tanga.
Akizungumza kwa niaba ya Mwenyekiti wa Bodi, Mwenyekiti wa Kamati ya Nishati, Mhandisi Ngosi Mwihava, ameeleza kuridhishwa kwa bodi na maendeleo ya mradi huo.

Amesisitiza kuwa EWURA ina jukumu la kusimamia utekelezaji wa mradi huu sambamba na kuhakikisha Watanzania wananufaika na fursa za ajira, uhamishaji wa ujuzi na teknolojia, pamoja na upatikanaji wa fursa za kibiashara zinazohusiana na utoaji wa bidhaa na huduma.
Akitoa ufafanuzi zaidi, Mkurugenzi wa Rasilimali Watu na Huduma za Utawala wa Kampuni ya EACOP, Geoffrey Mponda, amesema kuwa hadi sasa mradi huo umetoa ajira kwa watu zaidi ya 6,000, ambapo takriban asilimia 70 ni wakazi wa maeneo yanayozunguka mradi huo, jambo linaloonyesha kuimarika kwa ushiriki wa wazawa katika mradi huo.

Mapema kabla ya kutembelea mradi, Bodi ya EWURA ilikutana na Mkuu wa Mkoa wa Tanga, Balozi, Dkt. Batilda Salha Burian, ambaye ameeleza kuwa mradi wa EACOP umeleta manufaa makubwa kwa wakazi wa mkoa huo, na kwamba wazabuni wengi wa ndani wamejisajili kwenye kanzidata ya watoa huduma inayosimamiwa na EWURA.
Serikali ya Tanzania inamiliki asilimia 15 ya hisa za mradi kupitia Shirika la Maendeleo ya Petroli Tanzania (TPDC).
More Stories
TFS yawakaribisha wawekezaji katika vivutio vya utalii wa misitu
Waziri Bashungwa:Tumieni teknolojia za kisasa kudhibiti uhalifu unaovuka mipaka
Flightlink kuzindua Safari za Ndege za Kila Siku kwenda Nairobi wiki ijayo