May 24, 2025

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Dkt.Tulia atangaza kugombea Jimbo Jipya la Uyole

Na Esther Macha,TimesmajiraOnline,Mbeya

SPIKA wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ambaye pia ni Rais wa Umoja wa Mabunge Duniani(IPU) na Mbunge wa Mbeya Mjini,Dkt.Tulia Ackson,ametangaza nia ya kugombea Ubunge jimbo jipya la Uyole mkoani Mbeya katika Uchaguzi Mkuu utakaofanyika mwezi Oktoba mwaka huu.

Dkt.Tulia amesema hayo leo 23 Mei,2025 alipokuwa akihutubia Mkutano Mkuu Maalum wa Wilaya ya Chama Cha Mapinduzi (CCM), ambapo amesema kuwa ameamua kufanya uamuzi huo ili kuwahudumia wananchi wa Uyole kutokana na kasi ndogo ya maendeleo iliyopo katika eneo hilo.

“Maendeleo ya Uyole yanasonga kwa taratibu sana,nimeona ni vyema nijitoe kwa moyo wote kuhakikisha wananchi wa Uyole wanapata huduma stahiki na maendeleo ya haraka.Nitoe wito kwenu, watu wengi watakuja kwenu, chagueni kiongozi, chagueni mtumishi, itasaidia sana kuendelea kuyakimbiza maendeleo ya jamii,”amesema Dkt.Tulia.

Awali amezishukuru Kata zote thelathini na sita kwa ushirikiano mkubwa waliompatia wakati akitekeleza majukumu yake na kusema maendeleo yanapoletwa katika jamii kuna watu wananufaika na wengine wanapata maumivu.

Aidha  Dkt.Tulia amesema kugawanywa kwa Jimbo ni kusogeza maendeleo kwa wananchi na maombi yalikuwa mengi nchini lakini mkoa wa Mbeya ni miongoni mwa majimbo nane yaliyogawanywa.

Dkt.Tulia amesema katika kuhakikisha maendeleo yanasonga mbele atahakikisha majimbo yote mawili yanapaa kimaendeleo na kusema bado ni mzazi wa watoto wote wawili.

Aidha  Dkt.Tulia amesema kuwa Kwa mgawanyiko huo wa Jimbo asiwepo mtu wa kujiona ni zaidi ya mwenzie na kutoa wito kwa wananchi wa Mbeya Mjini kuchagua Viongozi bora wenye hofu ya Mungu watakaochagiza maendeleo.

Kwa upande wake Mwenyekiti wa Chama cha Mapinduzi Wilaya ya Mbeya Mjini ,Afrey Nsomba amesema kuwa  Dkt.Tulia amekuwa kiongozi wa mfano , wanawake,vijana na kusema kila siku amekuwa ni daraja,na habagui na kujali makundi yote.

“Leo hii kazi nyingi ulizofanya wewe kama mbunge wetu  na ndo maana hapa kila mmoja hapa anavutia upande wake  lakini kitendawili hiki utakitegua mwenyewe,mh Mbunge sisi wana mbeya  tunakupenda Sana na Mimi niseme kama mwrnyewekiti kokote utakokwenda lazima upite kwa kishindo kikubwa lazima heshima yako iendelee kusimama,kwani umefanya Mbeya yetu kuwa na mabadiliko makubwa”amesema Mwenyekiti huyo.

Akizungumza katika mkutano huo Maalum, Mwenyekiti wa Chama cha Mapinduzi Mkoa wa Mbeya, Patrick Mwalunenge amesema kuwa  Dkt Tulia amekuwa mtu wa kujali watu na kujitoa hivyo ni jambo ambalo linahitaji moyo wa kipekee Sana na kwamba wana Mbeya wanatakiwa kumpa ushirikiano popote atakapokuwa anaenda.

“Kama chama tunakuhakikishia tutakupa ushirikiano mkubwa kwasababu kazi zako zinajieleza na tutahakikisha unarudi tena kwa kishindo kikubwa,”amesema.