Na Yusuph Mussa,Timesmajiraonline,Arusha
MAKAMU wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt.Philip Mpango, amezindua rasmi Shule ya Sekondari ya Mfano ya Benki ya CRDB, itakayojengwa katika Halmashauri ya Jiji la Dar es Salaam kama sehemu ya maadhimisho ya miaka 30 ya Benki ya CRDB, ambapo shule hiyo ya kisasa ni matokeo ya dhamira ya benki hiyo ya kuunga mkono juhudi za Serikali katika kuwekeza kwenye elimu bora kwa watoto wa Kitanzania.
Akizungumza leo Mei 16, 2025 wakati wa uzinduzi wa shule hiyo uliofanyika katika Seimna ya Wanahisa wa Benki ya CRDB kuelekea Mkutano Mkuu wa 30 wa Wanahisa utakaofanyika kesho Mei 17, 2025 Ukumbi wa Simba Kituo cha Mikutano cha Kimataifa Arusha (AICC) jijini Arusha, Dkt. Mpango aliipongeza Benki ya CRDB kwa mchango wake mkubwa katika maendeleo ya kijamii, hususan sekta ya elimu.

“Nawapongeza kwa kuwa mfano wa kuigwa kwa sekta binafsi. Mmekuwa mstari wa mbele sio tu kwenye huduma za kifedha bali pia katika kuleta mabadiliko ya kweli kwenye jamii. Pia nawapongeza benki ya CRDB kwa kutimiza miaka 30 tokea kuanzishwa kwake mwaka 1996” alisema Dkt. Mpango.
Dkt. Mpango pia aliwapongeza Benki ya CRDB, kwani pamoja na kujenga shule hiyo ya kisasa, bado wanarudisha kwa jamii kile walichokipata ikiwemo huduma za jamii na shughuli za maendeleo, lakini pia na utunzaji wa mazingira, na kuzitaka taasisi nyingine kuiga yanayofanywa na benki hiyo, na kama wao CRDB wamejenga Dar es Salaam, wao wajenge kwenye mikoa mingine.
Akizungumza katika semina hiyo, Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi wa Benki ya CRDB, Dkt. Ally Laay alisema tangu kuanzishwa kwa benki hiyo mwaka 1996, imeendelea kuwa mshirika muhimu wa maendeleo kwa Taifa kwa kutoa huduma za kifedha zenye kugusa maisha ya wananchi moja kwa moja.

“Shule ya Sekondari ya Mfano ya Benki ya CRDB ina uwezo wa kuchukua wanafunzi zaidi ya 600 na itajengwa kwa viwango vya kisasa ikiwa na madarasa ya kisasa 16, maabara nne (4), maktaba moja, chumba cha TEHAMA kimoja, ofisi za walimu na wafanyakazi 11, vyoo 53, miundombinu rafiki kwa wanafunzi wenye mahitaji maalum, pamoja na maeneo rafiki ya michezo. Mradi huu unatarajiwa kugharimu takribani sh. bilioni tano” alisema Dkt. Laay.
Naye, Mkurugenzi Mtendaji wa Benki ya CRDB, Abdulmajid Nsekela, alisema shule hiyo ni zawadi ya benki kwa Watanzania katika kuadhimisha miaka 30 ya mafanikio ya benki hiyo.
“Tulipojiuliza ni zawadi gani ya kipekee tungeweza kuwapa Watanzania katika kutimiza miaka 30, tulikubaliana kwamba elimu ni urithi wenye nguvu kuliko wote. Shule hii ni ushahidi wa dhamira yetu ya kuwekeza katika kizazi kijacho.
“Shule hii ni sehemu ya mpango mpana wa Benki ya CRDB wa kurudisha kwa jamii katika nyanja za elimu, afya, mazingira na uwezeshaji wanawake kupitia CRDB Bank Foundation. Tunaamini kuwa maendeleo endelevu hayawezi kufikiwa bila uwekezaji wa makusudi katika elimu. Kupitia shule hii, tunaweka msingi wa taifa lenye maarifa, maadili na ushindani wa kimataifa” alisema Nsekela.
Akitoa salamu zake, Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, Profesa Adolf Mkenda aliishukuru Benki ya CRDB kwa mchango wake mkubwa katika maendeleo ya sekta ya elimu nchini.

“Kwa niaba ya Serikali na Wizara ya Elimu, naishukuru sana Benki ya CRDB kwa maono na uamuzi huu wa kujenga shule ya kisasa kwa ajili ya watoto wa Kitanzania. Huu ni mfano hai wa jinsi sekta binafsi inavyoweza kushirikiana na Serikali katika kujenga mustakabali bora kwa watoto na vijana wetu.” alisema Profesa Mkenda.
Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi wa CRDB Bank Foundation, Martin Warioba, alisema shule hiyo ni sehemu ya mkakati mpana wa Benki ya CRDB kuboresha mazingira ya elimu nchini na kufungua fursa kwa watoto wa Kitanzania, kwani mbali na kujenga shule hiyo ya mfano, pia wamejipanga kuanzisha mpango wa ufadhili wa masomo kwa wanafunzi wanaosoma masomo ya sayansi kwa kushirikiana na Wizara ya elimu.
Wanahisa wa Benki ya CRDB watafanya Mkutano Mkuu wa 30 kesho Mei 17, 2025, ambapo ajenda mbalimbali zinatarajiwa kujadiliwa ikiwamo kuidhinisha pendekezo la Bodi ya Wakurugenzi la gawio la shilingi 65 kwa hisa ikiwa ni ongezeko la asilimia 30 kulinganisha na gawio la shilingi 50 kwa hisa lililotolewa kwa mwaka 2023.

Takwimu zinaonesha, Benki ya CRDB ni moja ya benki zinazoongoza katika ukanda wa Afrika Mashariki, inatoa huduma kwa wateja wadogo, wakati na wakubwa ikiwamo huduma kwa wateja binafsi, huduma za hazina, huduma za bima, mikopo ya biashara, kilimo na uwezeshaji kwa wajasiriamali wadogo.
Benki ya CRDB ndio benki ya kwanza nchini Tanzania kutambuliwa na kampuni ya kimataifa ya utafiti ya Moodys Investors Service kuwa moja kati ya benki 10 imara na salama Afrika katika uwekezaji.
Moodys imeipa Benki ya CRDB daraja la uimara la B1 ambapo ni daraja la juu zaidi kupatikana kwa mabenki na taasisi za fedha katika ukanda wa jangwa la Sahara. Benki ya CRDB imekuwa kiungo muhimu cha biashara katika nchi za Tanzania, Burundi na Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo kwa kuwahudumia wateja zaidi ya milioni nne (4) na kupitia mtandao mpana wa matawi zaidi 260, zaidi ya CRDB Wakala 30,000, ATM 550, mashine za manunuzi 2,300 na Kituo cha Huduma kwa Wateja kinachotoa huduma saa 24 na siku saba kwa wiki

More Stories
Nsekela aeleza mafanikio miaka 30 Benki ya CRDB
Mhandisi Samamba ahimiza uaminifu kwa watoa huduma migodini
Mwanasheria Mkuu wa Serikali awataka wananchi kujitokeza kujiandikisha daftari la wapiga kura