May 10, 2025

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Mdiwani Bumbuli wataka jitihada ziongezwe ukusanyaji mapato

Na Yusuph Mussa,Timesmajiraonline,Bumbuli

BAADHI ya Madiwani wa Halmashauri ya Wilaya ya Bumbuli mkoani Tanga wamesema wameona jitihada zinazofanywa na halmashauri hiyo katika ukusanyaji wa mapato ya ndani tofauti na miaka ya nyuma, lakini wametaka jitihada hizo ziongezwe hasa kwa baadhi ya kata.

Waliyasema hayo Mei 6, 2025 kwenye kikao cha Baraza la Madiwani wa Halmashauri hiyo robo ya tatu, na kuitaja Kata ya Kwamkomole kuwa ipo nyuma sana kwenye kuchangia mapato ya ndani wakati huduma za kijamii na miradi ya maendeleo wanapata kutoka fedha za Serikali na halmashauri kupitia mapato ya ndani.

“Naipongeza halmashauri kwa jitihada zake inazofanya hasa kwenye makusanyo ya mapato ya ndani. Tulipotoka huko nyuma na sasa hivi ni tofauti, lakini wakati tunapongeza bado jitihada zinahitajika sababu tuna uwezo wa kukusanya zaidi ya haya tunayoyaona sasa. Kata ya Kwamkomole bado inaendelea kushika mkia kwenye ukusanyaji wa mapato ya ndani.
Kwamkomole wanaishi watu, wanakunywa pombe, wanafanya biashara, wana maduka, vioski na shughuli nyingine za kijamii.

“Kufanya biashara ni lazima wakate leseni ya biashara, na leseni ya biashara ni sehemu ya mapato ya ndani. Na tuliagizana kwenye vikao vyetu mapato ya ndani ni ajenda yetu ya kudumu kwenye Kamati za Maendeleo ya Kata (WDC). Sasa tunataka maelezo, ni kweli Kwamkomole hakuna duka hata moja linaloweza kulipia leseni ya biashara ya sh. 21,000 au kilabu cha pombe za kienyeji kinachoweza kuchangia sh. 7,000 kwenye mapato ya ndani, sababu Kwamkomole wananchi hawachangii chochote kwenye mapato ya ndani, ni sifuri” alisema Diwani wa Dule B, Ali Mkwavingwa.

Diwani wa Kata ya Kwamkomole Hozza Mandia aliwataka Wakala wa Barabara Mijini na Vijijini (TARURA) kuweza kufanya matengenezo kwenye kipande cha barabara ya kutoka Soni kwenda Mponde eneo la Kijiji cha Magila, kwani kipande hicho cha mita 200  kinakwamisha shughuli za usafiri kwa wananchi wa maeneo hayo.

Akijibu hoja hiyo, Kaimu Meneja wa TARURA Wilaya ya Lushoto Mhandisi Shehe Udesi alisema barabara hiyo ya Soni- Mponde ipo kwenye matengenezo na Mkandarasi yupo kazini, ambapo anatengeneza barabara hiyo kwa urefu wa kilomita sita kati ya 13 ya barabara hiyo kutoka Soni- Mponde. Ila kwa sasa amesimama kufanya kazi kutokana na mvua nyingi, lakini baada ya mvua kupungua, ataendelea na kazi hiyo.

Akijibu hoja za baadhi ya madiwani, Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Bumbuli (Bumbuli DC) Baraka Zikatimu alisema Kata ya Kwamkomole inakusanya mapato kupitia Service Levy kwenye zao la mkonge, ambapo wananchi wake ni wakulima wadogo wa zao la mkonge na wanalipa kwa Control Number. Na kuhusu wafanyabiashara kudaiwa kutolipa leseni za biashara, atafuatilia kuona mustakabali wake.

Wakati huo huo, Meneja wa Mfuko wa Taifa wa Bima ya Afya Mkoa wa Tanga Evance Nyangasi aliwaeleza madiwani wa Bumbuli umuhimu wa wananchi wao kujiunga na Bima ya Afya iwe kwa familia ya watu sita ama mtu mmoja mmoja. Na hiyo ni kutokana na Serikali kuamua kwa sasa Bima ya Afya itakuwa ni kwa wananchi wote.

Akizungumza na mwandishi wa habari hizi mara baada ya kikao hicho Diwani wa Kata ya Kwamkomole ambaye pia ni Makamu Mwenyekiti wa Halmashauri hiyo Hozza Mandia alisema kata yake inachangia mapato ya halmashauri kupitia zao la mkonge, huku akitanabahisha kuwa hata wafanyabiashara wake wa maduka wanalipia leseni.

“Kata ya Kwamkomole inalipa ushuru na kodi ya Serikali. Wananchi wa Kwamkomole wanalima mkonge, na ushuru wa zao la mkonge unalipwa kwa Control Number tofauti na kutumia POS, na ndiyo maana mapato hayaonekani kwenye taarifa, lakini kwenye kikao cha Baraza la Madiwani cha Taarifa za Kata, ushuru wa Kata ya Kwamkomole utaonekana kwenye taarifa. Hata leseni wananchi wanalipa, lakini huu sio wakati wa kulipa leseni ndiyo maana haionekani kwenye taarifa” alisema Hozza.