May 1, 2025

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Dawasa, DPC kuimarisha ushirikiano

Na Mwandishi wetu, Timesmajira Online.

MAMLAKA ya Maji Safi na Usafi wa Mazingira Dar es Salaam (Dawasa), imesema iko tayari kuimarisha ushirikiano na klabu ya wanahabari wa Mkoa wa Dar es Salaam (DPC), kwa ajili ya kujenga uelewa kuhusu shughuli zake na kutoa elimu kwa umma.

Akizungumza katika kikao maalumu baina yake na uongozi wa DPC jijini Dar es Salaam, Mkuu wa Kitengo cha Mawasiliano Dawasa, Everlasting Lyaro amesema mamlaka hiyo inatambua mchango mkubwa wa wanahabari katika kuelimisha na kuhabarisha umma, kwa ajili ya kujenga uelewa mpana wa shughuli za kila siku za maendeleo.

Amesema, mchango wa wanahabari katika maendeleo ya Jiji la Dar es Salaam na viunga vyake ni mkubwa ambao haupaswi kupuuzwa na kwamba katika siku zijazo, Dawasa itaendelea kuimarisha uhusiano wake na DPC kwa ajili ya kufikisha taarifa kwa wananchi kwa wepesi.

“Dar es Salaam bado inaendelea kuwa Jiji namba moja la kibiashara, mchango wake kwa Taifa ni mkubwa. Watumiaji wa huduma zetu wanaendelea kuongezeka kila siku. Sisi pia tunaendelea kuboresha huduma zetu ili kukidhi mahitaji ambayo yanaongezeka kila siku.

Mkuu wa Kitengo cha Mawasiliano Dawasa, Everlasting Lyaro (kushoto), akimkabidhi diary Kaimu Mtendaji Mkuu wa DPC, Andrew Msechu (katikati), alipotembelea ofisi za klabu ya wanahabari Mkoa wa Dar es Salaam, hivi karibuni kwa ajili ya kujenga mahusiano. Kulia mjumbe wa bodi wa klabu hiyo Hamisi Miraji

“Tunaamini kwamba kwa kutumia kalamu za wanahabari inakuwa rahisi kuwafikia wananchi kwa wakati kwa ajili ya kueleza maboresho yanayofanyika katika huduma zetu na utekelezaji wa miradi mikubwa ya kimkakati ili kurahisisha upatikanaji wa huduma zetu. Kwa hiyo hili ni jukwaa zuri na muhimu kwetu kuwafikia wananchi,” amesema Lyaro.

Ameeleza matumaini yake kwa uongozi wa DPC, akisema anaamini katika utendaji wenye matokeo chanya na kwamba katika kipindi hiki, mambo mengi yatafanyika ili kujenga Imani kati ya pande hizo mbili.

Kwa upande wake, Kaimu Mtendaji Mkuu wa DPC, Andrew Msechu amesema klabu hiyo yenye wanachama zaidi ya 194 kwa sasa imekuwa ikitoa kipaumbele katika utoaji wa elimu kwa wanachama wake, ili kupanua uelewa kuhusu shughuli za taasisi na mashirika mbalimbali, kwa ajili ya kuimarisha daraja kati yao na wananchi.

Amesema, katika kujenga taswira ya DPC kwa umma, uongozi umejipanga kuhakikisha wanatimiza malengo yaliyowekwa, ikiwemo kujenga uhusiano mzuri na wadau wote wa habari na maendeleo, ili kujenga kesho iliyo bora kwa wadau na wanachama wake.

“Tuko katika kipindi ambacho mchango wa wanahabari unatakiwa uthaminiwe na wanahabari wenyewe wanatakiwa kuhakikisha wanatimizawajibu wao ipasavyo.

“Jukumu letu kubwa ni kuwaunganisha na kujenga uwezo na uelewa kuhusu mambo mtambuka, kwa hiyo hatua hii ni muhimu sana kwetu. Tuna mani tutaenedelea kujenga mashirikiano baina yetu na Dawasa katika namna ambayo itazisaidia pande zote mbili,” amesema Msechu.